Wizara ya Afya, Tamisemi na Muhimbili wakabili uhaba wa watalaamu dawa za usingizi na ganzi nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akikabidhi cheti Bw. Craft Ditick Ng’itu kutoka Mkoa wa Lindi, Halmashauri ya Mtama katika kituo cha Afya cha Nyanganala. Bw. Ng’itu ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya kutoa dawa za usingizi na ganzi kwa wagonjwa katika vyumba vya upasuaji. Wataalamu hao wametoka katika mikoa mbalimbali nchini katika ngazi ya wilaya na vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa mafunzo hayo kwa muda wa miezi sita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na wahitimu hao kabla ya kuwakabidhi vyeti.

Baadhi ya wahitimu wakimsikiliza Prof. Museru katika hafla ya kuwaaga wataalamu hao.

Wataalamu wa MNH wakiwa kwenye hafla hiyo.

Mkuu wa Idara ya Usingizi wa Muhimbili, Dkt. Moses Mulungu akizungumza na wataalamu hao kuhusu kuzingatia utaalamu waliopatiwa wakati wa kuhudumia wagonjwa mara watakaporejea kwenye vituo vyao vya afya.

Wataalamu wakifuatilia hafla hiyo.

Prof. Museru akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu waliotihimu mafunzo ya dawa za usingizi na ganzi.


Na John Stephen

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameendelea kutoa mafunzo ya watalaamu wa dawa za usingizi na ganzi kutoka vituo vya afya na Hospitali za Wilaya nchini zenye uhaba huo ili ziweze kutoa huduma ya upasuaji.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru wakati akiwatunuku vyeti wahitimu 48 waliopata mafunzo ya utoaji dawa za usingizi pamoja na ganzi yanayotolewa na hospitali kwa kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja.

“Mtakumbuka kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya nchini kuanzia ngazi ya taifa hadi kwenye zahanati. Kutokana na mageuzi hayo kumekuwa na uhaba wa watalaamu wa dawa za usingizi na ganzi hivyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Tamisemi zilikuja na mpango wa kusomesha watalaamu hao ngazi ya cheti watakaosaidia kutoa huduma hiyo kwenye  vituo vya afya na hospitali za wilaya zenye uhaba huo,” amesema Prof. Museru.

Ameeleza kuwa katika jitihada hizo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo MNH waliandaa mtaala wa mafunzo hayo maalumu kwa watalaamu wa dawa za usingizi na ganzi ambapo Tamisemi inaleta watalaamu kutoka sehemu mbalimbali nchini kutoka vituo vya afya na hospitali za Wilaya ili kujifunza na kuwalipia gharama za mafunzo pamoja posho za kujikimu.

“Tangu tumeanza programu hii zaidi ya miaka sita iliyopita, tumefundisha zaidi ya wataalamu 400 kwa Dar es Salaam na mikoa jirani ambapo kati yao watalaamu zaidi ya 150 wametoka Halmashauri mbalimbali nchini. Nafurahi pia katika kundi hili la wahitimu 48 baadhi yao wametokea Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya kutoka Mafia, Lindi, Mtama, Rufiji, Kasulu, Kibondo na maeneo mengine na zoezi hili ni endelevu,” amesema Prof. Museru.

Amewahimiza kufanya kazi kwa weledi na kujituma watakaporudi vituo vyao vya kazi ili kuonesha mabadiliko ya uwepo wao baada ya mafunzo.

“Mmepata mafunzo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili inayotoa huduma za ubingwa na za kibobezi hivyo kujifunza mafunzo yenu kwa viwango vya juu. Mmepita kwenye mikono ya watalaamu waliobobea na mmepikwa vizuri kitalaamu nendeni mkawatumikie wananchi kwa weledi,” amesisitiza Prof. Museru.

Amesema kuna baadhi ya ama Vituo vya Afya au Hospitali kulikua na madaktari wanaoweza kufanya upasuaji lakini hawakuwa na watalaamu wa dawa za usingizi na ganzi hivyo kusababisha wananchi kufuata huduma ya upasuaji kwa kusafiri umbali mrefu kwenda penye watalaamu hao hali iliyokuwa inachelewesha huduma, kumuongezea mwananchi gharama na wakati mwingine kusababisha matokeo ya upasuaji kutokuwa mzuri.

Watalaamu hawa wa dawa za usingizi na ganzi wanatofautiana kwenye viwango vya elimu kuanzia ngazi ya cheti, diploma, udaktari na udaktari bingwa na aina ya upasuaji unaofanyika. Ndiyo maana mtaalamu huyu hawezi kutoa dawa za usingizi kwa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa ubongo, figo au mapafu bila usimamizi wa daktari bingwa. Hata hivyo aina hii ya upasuaji haipatikani ngazi ya kituo cha afya au hospitali ya Wilaya bali Hospali za Rufaa za Mkoa, Kanda na Taifa zenye madaktari bingwa wa upasuaji wa aina hiyo.

Prof. Museru amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) imeboresha huduma zake kwa viwango vya ubingwa na ubobezi hivyo anazialika Hospitali zote nchini ngazi ya kanda, mkoa, wilaya na vituo vya afya kuendelea kuitumia ili kufundisha watalaamu wake katika maeneo mengi ambayo wana changamoto ama ya watalaamu, ujuzi na uanzishwaji wa huduma mpya katika maeneo hayo ambapo hili ni jukumu la msingi ambalo Muhimbili tumekabidhiwa kulifanya hapa nchini.