Waziri Ummy azindua mtambo wa kuzalisha hewa tiba Mloganzila

Balozi wa Korea Kusini Nchini Mh. Kim Sun Pyo (wa pili Kushoto) akikabidhi hati ya makabidhiano ya Mradi wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant) kwa Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu (wa Pili kutoka kulia)

Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu (Katikati) na Balozi wa Korea Kusini Nchini Mh. Kim Sun Pyo wakikata utepe kuzindua mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant).

Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu (Wa pili kutoka kushoto) akikagua Wodi ya Watoto Wachanga wanaohitaji Uangalizi Maalumu (NICU) iliyoboreshwa kwa ufadhili wa KOFIH.

Mh. Ummy Mwalimu akizungumza katika hafla ya Makabidhiano ya Mradi

Balozi wa Korea Kusini Nchini Mh. Kim Sun Pyo akizungumza katika hafla ya Makabidhiano ya Mradi

Naibu Mkurugenzi Mtendaji Muhimbili Mloganzila akizungumza katika hafla ya Makabidhiano ya Mradi.

Baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo wakisikiliza hotuba


Na Sophia Mtakasimba

Waziri wa Afya Mh. Ummy mwalimu amezindua  mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant) wenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya ujazo wa 6.3 M³ kwa siku  ambao umegharimu  dola za Marekani 300,000,  pamoja na mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto uliohusisha Uboreshaji wa  wodi ya watoto wachanga mahututi (NICU) Pamoja na kuanzisha Wodi ya Uangalizi Maalumu ya Wazazi (Maternal ICU) kwa gharama TZS 240,808,060 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila.


Mtambo wa kuzalisha hewa tiba ambao ulioanza  kutumika tangu  Januari mwaka huu una tanki lenye ujazo wa lita 4000 ambalo limeunganishwa moja kwa moja kwenye matumizi ya kila siku ya hospitali wakati wodi ya Watoto Wachanga wanaohitaji uangalizi maalumu (NICU) ikiwa imeongeza uwezo wa kulaza kutoka watoto 30 hadi watoto 60 na maternal ICU ina vitanda vya Wagonjwa Mahututi 4 na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu 6. Miradi yote hii imefadhiriwa na Korea kupitia Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH)


“Nitumie fursa hii kwa niaba ya serikali kuipongeza serikali ya Korea kupitia KOFIH kwa msaada huu mkubwa ambao utasaidia kuimarisha afya za watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanaokuja kupatiwa matibabu hapa Mloganzila kwa kuwa hii ni hospitali ya rufaa. Ufadhili wa miradi hii unaendelea kudhihirisha uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali ya Tanzania na Serikali ya Korea Kusini” Amesema Mh. Ummy


Waziri Ummy alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita pamoja na mambo mengine imedhamiria kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kuboresha miundombinu na kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vifaa saidizi na vitendanishi kulingana na mahitaji katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020.

Katika hatua nyingine Mh. Ummy amesema imefika wakati sasa wa hospitali ya Mloganzila kujitegemea na kusimama yenyewe kwa kuwa sasa inajiweza tofauti na ilivyokuwa awali.


“Nimeshatoa maagizo kwa katibu mkuu kwamba kuanzia Julai Mosi Hospitali ya Mloganzila ianze kujitegemea yenyewe, kwa kipindi cha miaka minne imekuwa chini ya uangalizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, sasa imetosha.


Aidha Mh. Ummy amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru kwa usimamizi mzuri wa Hospitali ya Mloganzila.

“Hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi lakini kwa sasa idadi ya wananchi wanaopata huduma imeongezeka hii inaonyesha hospitali hii kwa sasa imekuwa na inaweza kujitegemea” amesema Mh. Ummy
Awali akiwasilisha taarifa ya miradi hiyo kwa Waziri, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Muhimbili Mloganzila Dkt. Julieth Magandi alisema kuwa mbali na miradi hiyo mikubwa miwili pia KOFIH imefadhili ukarabati wa karakana ya Vifaa tiba (Bio Medical workshop).


Akielezea Faida za uwepo wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant) hospitalini hapo Dkt. Magandi amesema kuwa ni pamoja na kuokoa fedha nyingi ambazo hospitali ilikuwa inatumia kununua gesi kwa wazabuni


“Uwepo wa mradi huu umeweza kuokoa TZS 33,000,000 kwa mwezi ambazo zilikuwa zinatumika kununua hewa tiba kutoka kwa wazabuni. Aidha, hospitali inatumia mtambo huu kuongeza kipato chake kwa kuuza mitungi ya ziada kwa taasisi nyingine. Mfano hadi tarehe Machi 16, 2022 jumla ya mitungi 1520 imeuzwa Muhimbili-Upanga” amesema Dkt. Magandi
Kuhusu Mipango ya baadaye ya Hospitali Dkt. Magandi amesema ni pamoja na kujenga jengo la upandikizaji viungo (Transplant Centre), kuhamisha tanki la maji taka kwenda nje ya jengo, kujenga jengo maalumu la kufulia kutokana na lililopo sasa kuwa finyu na kuendelea kutoa motisha kwa wafanyakazi ili kuchochea tija ya uwajibikaji.