WAZIRI MABULA AIPONGEZA MUHIMBILI KUVUNJA MAWE KWENYE FIGO KUPITIA MAWIMBI MSHITUKO

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Angeline Mabula akifanyiwa uchunguzi wa macho.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Angeline Mabula akipima uzito wake.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Angeline Mabula akisaini kitabu cha wageni katika banda la Muhimbili.


Na Neema Wilson Mwangomo

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Angeline Mabula ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kutoa huduma ya matibabu ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko kwa kitaalam bila kufanya upasuaji.

Waziri Mabula amesema hayo baada ya kutembelea banda la Muhimbili kwenye maonesho ya 44 ya SABASABA na kufuraishwa na huduma zinazotolewa kwa wananchi ambapo yeye mwenyewe alipata fursa ya kupima macho, shinikizo la damu bila malipo pamoja na kupata elimu ya afya.

Amesema kuanzishwa kwa matibabu haya ni mwendelezo wa kutekeleza juhudi za Serikali za kuboresha huduma bobezi za kibingwa nchini ili kuongeza wigo wa huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani hapa nchini kutokana na kutokuwepo kwa wataalamu, vifaa tiba au vyote viwili.

Huduma hii inafanywa kwa kutumia mashine ambayo inatoa mawimbi sauti yanayosafiri kupitia ngozi hadi kwenye figo sehemu yenye jiwe au mawe. Mawimbi hayo hugeuka kuwa nishati yenye uwezo wa kuvunja mawe kuwa madogo mithili ya mchanga ambapo yakishasagwa yanatoka kwa njia ya haja ndogo ( mkojo).