Wauguzi wasisitizwa kuzingatia maadili ya kazi

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini Sista Agnes Mtawa (kushoto) akimkabidhi Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila Dk. Julieth Magandi kitabu cha maadili na miongozo ya wauguzi na wakunga, leo hospitalini hapo.

Mratibu wa leseni na Maadili Sista Jane Mazigo akitoa mada katika mafunzo ya siku moja ya kuwaongezea ujuzi wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Mloganzila.

Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wakimsikiliza Mratibu wa leseni na maadili Wakati akitoa mada katika mafunzo hayo.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila Dk. Julieth Magandi (watatu kutoka kulia aliyevaa koti jeupe) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukungu nchini Agnes Mtawa (watatu kutoka kushoto aliyevaa gauni la bluu) pamoja na washiriki wengine wa mafunzo hayo.


Na Abubakary Mahamoud Omary

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukungu nchini Agnes Mtawa amewataka wauguzi na wakunga kuzingatia maadili ya kazi ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Sista Mtawa amesema hayo leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza katika mafunzo ya siku moja ya kuwaongezea ujuzi wauguzi na wakunga   wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila sambamba na kuwakumbusha maadili ya kazi.
“Katika kutoa huduma tuna maadili (Professional Code of Conduct) na miongozo (The Guiding Principle) ambayo kila muuguzi na mkunga anatakiwa afuate hizo taratibu kwakua jamii inawategemea katika usimamizi na utoaji wa huduma bora” amesema Sista Mtawa.
Pia amesisitiza kwamba kila muuguzi na mkunga anapaswa kuwa na leseni hai inayompa nafasi ya kutoa huduma kwani kutokuwa na leseni hai ni kosa na mtoa huduma anaweza kupoteza kazi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa Hospitali ya Mlogaznila Sista Redamptha Matindi ameshukuru kutolea kwa mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo wauguzi wa hospitali hiyo.