Wauguzi wakumbushwa kuzingatia maadili ya kazi

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa akiwaapisha wauguzi kwenye maadhimisho ya Siku ya Uuguzi Duniani ambayo hufanyika Mei 12, kila mwaka. Leo wauguzi wameapishwa kukumbushwa kutoa huduma kwa kuzingatia kanuni na taratibu kama walivyojifunza. Wengine kushoto ni viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na viongozi wa Chama cha Uuguzi na Ukunga Tanzania (TANNA) wakishiriki katika shughuli ya kuwaapisha wauguzi leo.

Baadhi ya wauguzi wakishiriki kuapa katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani ambayo hufanyika Mei 12, kila mwaka.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Bw. Makwaia Makani akizungumza na wauguzi leo katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani.

Waauguzi wakimsikiliza Bw. Makani wakati alipokuwa akizungumza nao leo.

Mmoja wa washiriki, Bi. Mwanahamisi Mvimba akiwasilisha mada kuhusu ‘Sababu zinazochangia maambukizi kwenye vidonda kwa watoto walioungua moto’.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Bi. Redemptha Matindi akishiriki kuwasha mshumaa ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya uuguzi na ukunga duniani.

Mshiriki, Bi. Sofia Sanga akitoa mada kuhusu wauguzi kuzingatia taratibu na maadili wakati wa kuwahudumia wagonjwa.

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa akiwa katika picha ya pamoja na wauguzi na wakunga kwenye maadhimisho ya siku ya uuguzi duniani.


Na John Stephen

Wauguzi wametakiwa kuendelea kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kitaaluma kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa. 

Wito huo umetolewa leo na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa katika maadhimisho ya siku ya Uuguzi na Ukunga Duniani ambayo yamefanyika Hopistali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuudhuriwa na wauguzi na wakunga wa MNH na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).     

Maadhimisho hayo hufanyika Mei 12, kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi Sauti inayoongoza Afya kwa Wote.” Mwaka huu kitaifa maadhimisho yanafanyika mkoani Katavi.

Bi. Mtawa amewakumbusha wauguzi kuzingatia mafunzo yanayotolewa mahala pa kazi kwani ndio yanayochochea kutoa huduma bora ya afya kwa wagonjwa.

Amewataka wauguzi kutambua kwamba huduma wanayotoa kwa wagonjwa ni huduma ya kibinadamu kwani elimu inachangia kufikia malengo ya kutoa huduma bora.

“Hivi sasa mambo yetu yanakwenda vizuri. Malalamiko mengi yamepungua kwani ukifuatilia utabaini kwamba malalamiko mengi ni ya wagonjwa au mgonjwa kutaka kupewa kipaumbele kupata huduma ya afya badala ya kufuata utaratibu,” amesema Bi. Mtawa.

Pia, Msajili amewapongeza wauguzi kwa kutekeleza majukumu ya kutoa huduma za afya kwa kuzingatia taratibu za kitaaluma kwa asilimia 100.

Akisoma risala katika maadhimishisho, Katibu wa Chama cha Uuguzi na Ukunga Tanzania, tawi la Muhimbili, Bw. Seif Hamisi ameomba vitendo vya udhalilishaji kwa wauguzi vifanyiwe kazi kwa kuwa vitendo hivyo vinawapunguzia ari ya kufanya kazi.

Kupitia risala, Katibu ameishukuru Muhimbili kwa kuwapatia wauguzi mafunzo mbalimbali ambayo yamewasaidia kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Bw. Makwaia Makani amewataka wauguzi kutoa taarifa kwa uongozi wa MNH endapo watadhalilishwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.

“Mmesikia jamani nendeni mkawaeleze wenzenu kwamba endapo muuguzi atadhalilishwa, bila kuchelewa naomba atoe taarifa kwa uongozi ili wanaofanya hivyo tuwafikishe mbele  ya vyombo vya dola,” amesema Bw. Makani.