Wauguzi na Wakunga Muhimbili Wanolewa
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Mhuhimbili Bi. Zuhura Mawona akifungua mafunzo kwa Wakunga na Wauguzi iliyoendeshwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC)
Muuguzi Kiongozi Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Bi.Joyce Mbura akitoa mada wakati wa mafunzo hayo
Afisa Muuguzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) Bi.Jackline Wambura akiwasilisha mada.
Baadhi ya Wauguzi na Wakunga wakifuatilia mafunzo
Baadhi ya Wauguzi na Wakunga wakifuatilia mafunzo
Na Irene Thomson
Wauguzi, Wakunga pamoja na Wauguzi Tarajali wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Upanga wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi zinazokubalika wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa mbalimbali wanaofika kupata matibabu katika hospitali hiyo.
Hayo yalisemwa na Muuguzi Kiongozi Mkoa wa Dar es Salaam, Bi.Joyce Mbura alipokua anafungua semina ya siku moja iliyolenga kuwakumbusha wauguzi kuhusu maadili ya taaluma pamoja na kujifunza mfumo mpya wa kuhuisha na kuhakiki leseni za wauguzi hao iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Wauguzi na Wakunga (TNMC).
Bi. Mbura aliwataka wauguzi kuzingatia sheria na kanuni ya Uuuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 ambayo ndio inatoa miongozo inasimamia taaluma ya Ukunga na Uuguzi.
“Wauguzi na wakunga mnapaswa kuwa na upendo na huruma kwa wagonjwa ,ndugu na jamaa wa wagonjwa wanaofika hapa kupata huduma na mnatakiwa kutoa huduma kwa wakati na pia kuboresha mawasiliano ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea” alisema Bi. Mbura
Kwa upande wake Afisa Muuguzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) Bi.Jackline Wambura wakati akitoa mada alisisitiza kuboresha huduma kwa wateja ili kuepusha malalamiko na pia kuzingatia haki, usalama, usiri, imani, mila na desturi ambazo haziathiri afya ya mgonjwa wakati wa utoaji huduma.
Pia, alisisitiza umuhimu wa wauguzi na wakunga kujiendeleza katika mafunzo mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanaoendelea duniani kote. .
Katika semina hiyo wataalamu hao pia walielekezwa namna wa kutumia mfumo wa kuhuisha na kuhakiki leseni zao pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuhuisha leseni na taratibu nyingine za mfumo.