Wauguzi Muhimbili watakiwa kuendelea kujituma

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akizungumza na wauguzi katika kikao kazi maalumu kilichofanyika Muhimbili.

Mkurugenzi wa Uuguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili Bi. Zuhura Mawona akizungumza na wauguzi katika kikao kazi maalumu kilichofanyika Muhimbili.

Baadhi ya Wauguzi wakimsikiliza Prof. Lawrence Museru

Muuguzi Anorld Nyanana kutoka jengo la Sewa Haji akichangia jambo wakati wa kikao kazi


Na Sophia Mtakasimba & Angela Mndolwa

Wauguzi hospitali ya Taifa Muhimbili wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi mkubwa ili kuweza kuifanya Hospitali kuendelea kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora za afya kwa watanzania .

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru wakati wa kikao kazi  na wauguzi hao.

Prof. Museru alisema kuwa ameona ni wakati muafaka kukutana na wauguzi ili kuweza kuongea na kubadilishana mawazo na kupata mrejesho wa mambo mbalimbali  yaliyofanyika.

"Asilimia 50 ya watumishi Muhimbili ni wauguzi , hivyo hospitali inategemea nguvu kazi hii ili kuweza kufikia dira na dhima yake ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi lakini pia kuwa kitovu cha wataalamu wa afya kujifunza "amesema Prof Museru.

Prof. Museru amesema kuwa anatambua kuwa kuna changamoto mbalimbali ambazo wauguzi wanakabiliana nazo ikiwemo upungufu na vitendea kazi lakini hospitali imejitahidi kuhakikisha kuwa inazipunguza changamoto hizo kwa kiasi kikubwa .

"Kwa ukubwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili changamoto haziwezi kuisha , na tumekuwa tukizipunguza kwa kadri hali inavyoruhusu, hivyo nawaomba changamoto ndogo zilizopo zisije zikaturudisha nyuma katika utendaji kazi wetu wa kila siku" amesema prof. Museru

Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa sana huduma za Hospitali zimeboreshwa sana na hilo limefanya watumishi kuwa na ari ya kujituma na kupelekea malalamiko kupungua na sasa wananchi wanafurahia huduma za Muhimbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uuguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili Bi.Zuhura Mawona amewataka wauguzi wote kuzingatia tunu tano ambazo ni uadilifu , heshima,uwajibikaji, ubora na usalama.

Akizungumzia mafanikio ya Kurugenzi ya Uuguzi Bi Mawona amesema kuwa kwa kushirikiana na wataalamu wengine wamefanisha kuanzishwa kwa huduma za kibingwa ikiwemo Kupandikiza Figo, kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia , na tiba Radiolojia

Lakini pia Hospitali imefanisha wauguzi kujiendeleza kimasomo ndani na nje ya nchi, pamoja na kuanzisha kiwanda cha ushonaji ambacho kilibuni vazi maalumu (PPE)la wataalamu kujikinga na Covid 19

Naye Anold Nyanana  ambaye ni muuguzi katika jengo la Sewahaji ameshukuru sana uongozi kwa  kuona umuhimu wa kutenga muda na  kukutana hivyo anaamini hata changamoto ndogo zitakazo kuwa zinajitokeza zitatatuliwa kwa wakati.