Watumishi watakiwa kuzingatia matumizi ya vifaa tiba.

Mkurugenzi wa Hospitali ta Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila Prof. Lawrence Museru akizungumza na Madaktari pamoja na Wauguzi kutoka Idara mbalimbali za MNH-Mloganzila ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma. Kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili- Mloganzila Dkt. Julieth Magandi.

Baadhi ya wauguzi wa wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wakati akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa katika maadhimisho hayo.

Mfamasia Bw. Thomasi Lukuba akitoa maoni yake juu ya upatikanaji wa dawa katika kikao cha madaktari na wauguzi ikiwa ni wiki maadhimisho ya Utumishi wa Umma.

Baadhi ya madaktari na wafamasia wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wakati akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa katika maadhimisho hayo.

Afisa Muuguzi Bw. Saidi Saidi akitoa maoni yake juu ya uboreshaji wa huduma za uuguzi hospitalini hapa

Dkt. Dismas Msemwa akitoa ushauri wa namna ya kuboresha mfumo wa Tehama hospitalini hapa.


Na Dorcas David

Watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wametakiwa kuzingatia umuhimu wa kutunza vifaa tiba ili viweze kutumika kwa muda mrefu kwakuwa gharama ya matengenezo ya vifaa hivyo ni kubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) Prof. Lawrence Museru ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wauguzi na madaktari  wa Hospitali ya Mloganzila ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika hospitalini hapa.

Prof. Museru amesema endapo kutakuwa na usimamizi mzuri wa matumizi ya vifaa tiba, hospitali itapunguza gharama za matengenezo na fedha hizo zitatumika katika shughuli nyingine za kuboresha huduma.

“Kifaa ili kidumu kinaanza na mtumiaji, ukipewa kifaa kitunze ili kiweze kukusaidia kufanya kazi yako kwa ufanisi, unapokikabidhi kwa mtoa huduma mwingine hakikisha kipo kwenye ubora unaotakiwa” amesisitiza Prof. Museru.

Aidha, Prof. Museru ameahidi kusimamia haki za watumishi na kueleza kuwa kila mmoja kwa nafasi aliyopo atapata haki yake, hivyo amewataka kufanya kazi kwa bidii kwani anatambua umuhimu wao kwa ustawi wa hospitali.

Katika hatua nyingine, Prof. Museru amesema Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) umekubali kuleta mabasi ya mwendokasi Mloganzila hatua ambayo itapunguza adha ya usafiri inayokawabili wananchi na wafanyakazi wanaokuja hospitalini hapa kila siku.

Prof. Museru amesema kwa sasa maandalizi stahiki yanaendelea ili kampuni hiyo iweze kuanza kutoa huduma za usafiri.

Wafanyazi wameupongeza uongozi wa Hospitali ya Muhimbili- Mloganzila kwa kutenga muda wa kuwasikiliza na kutoa ufafanunuzi wa changamoto mbalimbali na kuomba utamaduni huo uendelee hasa katika ngazi za idara.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya wiki ya Utumishi wa Umma inasema “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao utastawisha uongozi wenye maono hata katika mazingira ya migogoro”.