Watumishi tarajali Mloganzila watakiwa kuzingatia maadili ya kazi

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wa kada mbalimbali (tarajali), kushoto ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi

Baadhi ya wataalamu wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ambayo yametolewa leo katika Hospitali ya Mloganzila.

Afisa Muandamizi wa Takukuru Wilaya ya Ubungo Bi. Heavenlight Majule akiwasilisha mada juu ya namna ya kuzuia na kupambana na rushwa mahali pa kazi .

Afisa Maadili Muandamizi kutoka Ofisi ya Raisi Sekretarieti ya Maandali ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum ya Dar-es-salaam Bi. Mariam Nguzo akiwasisitiza watumishi tarajali kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma na kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuboresha huduma za afya .

Daktari Bingwa wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Garvin Kweka akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa mabadiliko ya tabia katika mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi.


Na Dorcas David

Wataalamu wa kada mbalimbali walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (tarajali) wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma ili kuendelea kuboresha huduma na kupata ujuzi utakao wawezesha kutoa huduma bora kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru wakati akifungua mafunzo kwa njia ya vitendo kwa watumishi tarajali wa Hospitali ya Muhimbili- Mloganzila.

Prof. Museru amesema wataalamu hawanabudi kuzingatia maadili ya kazi,kudumisha nidhamu na kufanya kazi kwa weledi ili kuepusha malalamiko juu ya utoaji wa huduma na kuongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja watafanya kazi chini ya uangalizi wa wataalamu wabobezi.

Naye Afisa Muandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Ubungo Bi. Heavenlight Majule amewataka wataalamu hao kufanya kazi kwa uaminifu, uwajibikaji na kuzingatia taaluma yao na kuepuka mazingira yatakayopelekea kupokea au kutoa rushwa wakati wa kutoa huduma.

“Jukumu lenu ni kutoa huduma iliyokuwa bora kwa jamii bila upendeleo na mnapaswa kufanya kazi kwa usawa na uwazi ili kuepuka kutengeneza mazingira ya takayopelekea kutoa rushwa” amesema Bi. Majule

Pamoja na hayo mesisitiza kuwa Takukuru haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa ikiwemo kupokea au kutoa rushwa mahali pa kazi.

Kwa upande wake Afisa Maadili Muandamizi kutoka Ofisi ya Raisi Sekretarieti ya Maandali ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum ya Dar-es-salaam Bi. Mariam Nguzo ametaja kanuni zinazowaongoza watumishi wa Umma kuwa ni kutoa huduma bora, utii kwa serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa Umma, kuheshimu sheria pamoja matumizi sahihi ya taarifa.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo huduma bora kwa wateja, kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na maadili ya utumishi wa Umma.