Watumishi Mloganzila wapatiwa mafunzo ya huduma bora kwa wateja

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru (katikati) akizungumza katika mafunzo ya huduma bora kwa wateja maadili na taaluma kwa watumishi wa Muhimbili-Mloganzila , kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Njoikiki Mapunda.

Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mloganzila wakiwa katika mafunzo ya huduma bora kwa wateja yaliofanyika leo.

Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga Bi. Sofia Sanga akitoa mada katika mafunzo ya huduma kwa wateja maadili na taaluma.

Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Bi. Martha Edward akielezea maana ya huduma bora kwa mteja na kutambua mteja ni nani.


Na Neema Wilson Mwangomo

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja ili kuwa mfano bora na wananchi  kuendelea kuwa na imani na huduma zinazotolewa na hospitali hii.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya huduma bora kwa wateja maadili na taaluma kwa watumishi wa Muhimbili-Mloganzila ambayo yamehusisha kada mbalimbali.

Prof. Museru ameeleza kuwa watumishi hawanabudi kutoa huduma bora kwa kuzingatia maadili ya kazi pamoja na miongozo ya utumishi wa umma ili wagonjwa waone fahari kupata huduma katika Hospitali ya Mloganzila.

Amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma na kuanzisha huduma mpya mbalimbali hivyo uboreshaji huu ni lazima uende sambamba na mabadiliko katika fikra zetu hasa tunavyowahudumia wateja.

“Awali kulikua na malalamiko ya huduma zisizoridhisha, lugha zisizostahili na kutowajali wateja malalamiko haya yamepungua kwa kisia kikubwa lakini bado tunawajibu wa kuendelea kutoa huduma inayostahili ili kumaliza kero zingine” amesema Prof. Museru.

Kutolewa kwa mafunzo haya ni utekelezaji wa agizo la serikali linalotaka kila taasisi ya Umma kutoa mafunzo ya huduma bora kwa watumishi wake sambamba na kuweka eneo maalumu la huduma kwa wateja ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

‘Serikali imekua ikisisitiza huduma bora kwa wateja ndiomaana tunawapatia mafunzo haya ambayo tuaamnini yataleta matokeo chanya katika utoaji huduma. Vilevile katika kutimiza agizo hili la serikali tayari tumeanzisha sehemu ya huduma kwa wateja  ambayo inatoa elimu kwa wateja wetu, inawaelekeza wateja wetu  , inapokea maoni na malalamiko na kisha kuyafanyia kazi” amesema Prof. Museru.

Akitoa mada Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga Bi. Sofia Sanga amesisitiza juu ya umuhimu wa kuheshimu utu, kutochelewesha huduma, lugha nzuri na kutoa taarifa kwa wateja pale huduma inapochelewa au kuahirishwa.