Watumishi Mloganzila wajitokeza kuchangia damu

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi la uchangiaji damu kwa watumishi leo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila.

Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mloganzila wakiendelea na zoezi la kuchangia damu lililofanyika leo hospitalini hapa.

Baadhi ya watumishi waliojitokeza wakisubiri kuchangia damu.


Na Dorcas David

Wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wamejitokeza kuchangia damu ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kujitolea ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kuwekewa damu  ikiwemo wakina mama wajawazito,watoto, majeruhi wa ajali na wagonjwa wa saratani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema mahitaji ya damu kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ni unit 40 hadi 60 kwa siku ukilinganisha na kiwango cha ukusanyaji damu  ambapo kwa siku hukusanywa unit 15 hadi 30 hivyo uhitaji bado ni mkubwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Magandi awali Muhimbili ilikuwa ikitegemea mgao wa damu kutoka Kitengo cha Damu Salama cha Taifa (NBTS), lakini kutokana na ongezeko la uhitaji  , Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wazee na Watoto  kwa kushauriana na uongozi wa mpango wa damu salama na uongozi wa Hospitali ya Muhimbili ulibariki mpango wa kuiwezesha timu  ya Kitengo cha Damu Salama Muhimbili kuweza kukusanya damu jijini Dar es salaam ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa wote wa hospitali  wanaohitaji damu.