Watoto wenye ulemavu wapokea msaada wa viti maalumu

Mkuu wa Idara ya Huduma za Uuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bw. Yassin Munguatosha (mwenye sare nyeupe) akipokea msaada wa viti maalumu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu kutoka upande wa kushoto kwa Winners Group, Fesal Foundation Zanzibar na Familia ya Augustine Tarimo. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Bw. Emmanuel Mwasota. Viti vingine vimekaliwa na watoto wakati makabidhiano yakiendelea.

Mkuu wa Idara ya Huduma za Uuguzi wa Muhimbili (MNH), Bw. Yassin Munguatosha akizungumza na wazazi wa watoto waliopatiwa msaada huo.

Baadhi ya wazazi wakisubiri kukabidhiwa msaada huo.

Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Bw. Emmanuel Mwasota akiwataka wazazi wa watoto kutunza viti walivyopokea.

Fesal Foundation Zanzibar, Winners Group na Familia ya Augustine Tarimo wakimsikiliza Bw. Mwasota.

Bw. Mohamed Bakari akishukuru baada ya watoto kupatiwa viti hiyo.

Baadhi ya watumishi wa MNH wakifuatilia utoaji wa msaada kwa watoto hao.

Wazazi na watoto wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Muhimbili.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa viti maalumu 15 vyenye thamani ya zaidi ya TZS 3 milioni na kuwapatia watoto wenye ulemavu ambao wanatibiwa hapa Muhimbili.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa Muhimbili, Mkuu wa Idara ya Huduma za Uuguzi Muhimbili, Bw. Yassin Munguatosha amewataka wazazi kutunza msaada huo ili wautumie kupeleka watoto hospitali na katika maeneo mengine kupata mahitaji mabalimbali.

“Naomba msichoke kutoa msaada kama huu kwani wapo watoto wengine wenye uhitaji mkubwa. Napenda kuwashukuru wote mliotoa viti hivi kwani mmetoa kwa moyo , wakati sahihi na kwa wahitaji sahihi,” amesema Bw. Mumguatosha.

Naye Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wa MNH, Bw. Emmanuel Mwasota amewataka wazazi kutumia viti hivyo kama walivyoelekezwa na si vinginevyo kwani baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia kuomba fedha mitaani.

 “Watoto ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu, hivyo mtapaswa kuwatunza watoto wenu kwani wengine wamekuwa wakiwafungia ndani na kukosa huduma za matibabu ambazo zinawasaidia kujihudumia wenyewe,” amesema Bw. Mwasota.

Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Bw. Muhamed Bakari ameshukuru Muhimbili na Feisal Foundation Zanzibar, Winners Group na Familia ya Augustine Tarimo kwa kuwapatia msaada huo.