WATALAAM TARAJALI WAFUNDWA MUHIMBILI

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiano kwa Umma na Huduma kwa Wateja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Bw. Aminiel Aligaesha akitoa mada kuhusu mawasiliano kwa watalaam wa afya walioko kwenye mafunzo ya njia ya vitendo (Tarajali).

Baadhi ya Watalaam wa afya walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (Tarajali) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu na Utafiti Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Faraja Chiwanga akiwasilisha mada kwa watalaam wa afya walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (Tarajali).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Hedwiga Swai (wa kwanza kushoto) akifuatilia uwasilishaji wa mada kwenye mafunzo hayo.


Na Sophia Mtakasimba

Watalaam wa afya walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (Tarajali), wametakiwa kutumia muda wao wa mwaka mmoja kujifunza na kupata ujuzi ili wanapomaliza waweze kujitegemea na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamezungumzwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Hedwiga Swai wakati akitoa nasaha za kuwakaribisha wataalamu wa afya 386 kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya nchini na nje ya nchi, ambao watafanya kazi chini ya uangalizi wa wataalamu wabobezi wa MNH.

Dkt  Swai amewataka wataalamu hao  kufanya kazi kwa bidii, maarifa na kutojihusisha na makundi yasiyokuwa na tija.

“Kila mmoja hapa amekuja kujifunza, ni muhimu kujiepusha na ulaghai na makundi na tunawategemea kujenga nidhamu ya kweli kwani ninyi ndio mtaenda kuhudumia wananchi baada ya kipindi cha mwaka mmoja wa mazoezi ya vitendo,” alisema Dkt. Swai.

MNH hupokea watalaamu tarajali zaidi ya 300 kila mwaka ambao hupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo katika idara mbali mbali za afya, lakini pia hupata fursa ya kujifunza katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Mifupa (MOI).

Naye mmoja wa wataalamu hao Bw. James Ernest Chepesi amesema kuwa matarajio yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa mafunzo hospitalini hapo ni kujifunza zaidi kwa kuwa hospitali ina vifaa tiba vya kutosha na inahudumia wagonjwa wengi kwa siku hivyo anaamini atapata fursa nzuri ya kujifunza zaidi.

Katika mafunzo haya mada kadhaa zimewasilishwa ikiwemo maadaili ya watalaam wa afya wawapo mazoezini, kujitambua, viwango vya huduma na mawasiliano kwa ujumla.