WATALAAM KUTOKA MUHIMBILI WAWASILI LINDI KUTOA HUDUMA ZA AFYA

Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Lindi Sokoine kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kuwajengea uwezo watalaam wa hospitali hiyo.

Madaktari Bingwa wa MNH pamoja na Madaktari wa Hospitali ya Sokoine wakiwa katika kikao cha asubuhi cha kiutendaji kabla ya kuanza kutoa huduma.

Wauguzi wa hospitali hiyo wakiwa katika kikao cha asubuhi kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali ya utoaji huduma za afya.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya kike na uzazi Geofrey Marandu akizungumza na mgonjwa ambaye amefika leo katika Hospitali ya Sokoine kwa ajili ya kupata huduma.

Dokta Willybroad Massawe ambaye ni Dkt. wa upasuaji , pua , koo na masiko (kushoto) pamoja na muuguzi Monica Mngoya (kulia) wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakimpatia maelezo mgonjwa ambaye amefika kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Lindi ambao wamejitokeza katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Lindi Sokoine wakisubiri kupatiwa huduma hii leo.


Na Neema Wilson Mwangomo

Madaktari Bingwa 11 pamoja na wataalam wengine wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) wamewasili katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Lindi Sokoine kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi wa mkoa huo sanjari na kuwajengea uwezo wataalam wa hospitali hiyo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya kike na uzazi kutoka MNH Geofrey Marandu amesema lengo la ujio wao katika hospitali hiyo ni kuwaongezea ujuzi watalaam wa hospitali za rufaa za mikoa nchini kupitia madaktari bingwa wa Muhimbili lakini pia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa Muhimbili.

‘’Hospitali imeweka mkakati wa kuzitembelea hospitali mbalimbali za rufaa za mikoa nchini ili kushirikiana nao katika kutoa huduma za afya  na kuwajengea uwezo , lakini pia kama Muhimbili tunatekeleza agizo la serikali linaloelekeza kupunguza  rufaa za wagonjwa kwenda kutibwa nje ya nchi hatua ambayo tayari MNH inaitekeleza hivyo utoaji wa huduma za fya kwa njia ya mkoba utasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Muhimbili endapo wangepewa rufaa ya kwenda kutibiwa huko’’.amesema Dkt. Marandu.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine Dkt. Jumanne Shija amesema ujio wa watalaam wa afya wakiwemo Madaktari Bingwa utainufaisha hospitali hiyo kwakua watalaam wake watajengewa uwezo kiutendaji na kupata ujuzi wa kutosha.

Ametaja maeneo ambayo wataalam wa hospitali ya Sokoine watanufaika na kujengewa uwezo ni upasuaji, magonjwa ya kike na uzazi, meno, macho, watoto, magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya koo ,pua na masikio pamoja na masuala ya maabara.

‘’Hii ni neema imetufikia watu wa Lindi natoa wito kwa wananchi wa mkoa huu na wale wa maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kuja kupata huduma, madaktari bingwa wamekuja ni lazima tuwatumie ili na tunufake na huduma za kibingwa zitakazotolewa kwa kipindi cha wiki moja watakachokuwepo hapa ‘’. amesema Dkt.Shija.

Kwa upande wao wananchi ambao wamejitokeza kupata huduma wameelezea kufurahishwa na ujio wa watalaam wa afya kutoka Muhimbili na kueleza kuwa ujio wao ni faraja kwa wananchi wa Lindi kwani watapata huduma za afya wakiwa katika maeneo yao na itawapunguzia gharama endapo wangepata rufaa kwenda Muhimbili kwakua ingewalazimu watumie gharama kubwa za usafiri na mahitaji mengine muhimu.