Wataalamu wakutana Mloganzila kujadili mbinu za kupambana na saratani ya matiti

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Caspar Haule akielezea sababu zinazochangia ugonjwa saratani ya matiti

Mmoja wa washiriki wa mafunzo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dkt. Meshack Shimweli akiwasilisha mada kuhusu hali ya saratani.

Baadhi ya wataalamu kutoka hospitali mbalimbali nchini wakifuatilia mada zinazowasilishwa katika mafunzo hayo .


Na Dorcas David

Wataalamu kutoka hospitali mbalimbali nchini wamekutana ili kuboresha huduma za upasuaji kwa wagonjwa wanaogunduliwa kuwa na saratani ya matiti ili kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Caspar Haule amesema mafunzo hayo yamejumuisha wataalamu wa Upasuaji, Radiolojia, Patholojia, Tiba ya Mionzi na Dawa, yamelenga kuwajengea uwezo kufanya upasuaji wa saratani ya matiti kwa kutoa uvimbe bila kuondoa titi lote kwa wagonjwa wenye dalili za mwanzoni.

Kwa mujibu wa Dkt. Haule satatani ya matiti inashika nafasi ya pili ikiongozwa na saratani ya mlango wa kizazi ambayo ndio tishio kubwa zaidi. 

 “Saratani ya matiti inashika nafasi ya pili duniani ikiongozwa na saratani ya mlango wa kizazi, mwaka 2019 hadi 2020 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tumewafanyia upasuaji wagonjwa wa saratani ya matiti 331, kati ya hao 32 tumewafanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe bila kuondoa titi au kuharibu muonekeno wa wake (Breast conserving surgery)”.amesema Dkt. Haule.

Ametaja baadhi ya sababu mbalimbali zinazochangia mtu kupata saratani ya matiti kuwa ni unene uliopitiliza, kurithi kutoka kwenye familia,utumiaji wa dawa za uzazi wa mpango pamoja na utumiaji wa dawa za kuongeza homoni ya kuzuia ngozi ya mwili kuzeeka au kusinyaa.

Hata hivyo Dkt, Haule amesema endapo ugonjwa wa saratani ya matiti ukigundulika mapema kabla haujasambaa kwenda sehemu mbalimbali za mwili unaweza kutibika na mgonjwa kuishi muda mrefu.

Mafunzo hayo yametolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Roche ya nchini Kenya ambapo yameshirikisha wataalamu 30 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga & Mloganzila, Temeke, Amana, KCMC, Bugando, Dodoma, Mbeya na Kenya.