Wataalamu wa tiba ya usingizi Mloganzila wahitimu mafunzo maalumu

Mkuu wa Idara ya Usingizi na Ganzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Phillip Muhochi (kulia) akimkabidhi cheti mhitimu wa mafunzo ya mwaka mmoja ngazi ya cheti ya kozi ya usingizi na ganzi Bw. Israel Mwasenga.

Viongozi wa Idara ya Usingizi na Ganzi wa MNH-Mloganzila katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo hayo.


Na Lightness Mndeme

Wataalamu sita wa tiba ya usingizi na ganzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wamehitimu mafunzo maalum ya mwaka mmoja ya ngazi ya cheti yaliyolenga kuwapatia ujuzi kuwapatia ujuzi wa namna ya kuhudumia wagonjwa wanaohitaji tiba hiyo.


Mafunzo hayo ambayo yametolewa na Hospitali ya Muhimbili kwa njia ya nadharia na vitendo kwa wataalamu ili kuwaongezea ujuzi na kisha kufanya mitihani mbalimbali ili kupima uwezo wao iwapo wanakidhi viwango vinavyohitajika kwa ajili ya kutoa huduma.


Mkuu wa Idara ya Tiba ya Usingizi na Ganzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Phillip Muhochi amesema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa kuzingatia viwango stahiki na kuwapatia wataalamu nafasi ya kwenda MNH-Upanga kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi.


“Mafunzo haya ya nadharia na vitendo yametolewa kwa viwango vya juu na kuwaruhusu wataalamu hawa kuzungukia maeneo ya mafunzo kama vile MNH-Upanga ili kuwapa uwanja mpana wa wao kujifunza na kupata ujuzi zaidi” amesema Dkt. Muhochi.


Sambamba na hilo Dkt. Muhochi ameongeza kuwa kutokana na uanzishwaji wa huduma mbalimbali zinazohitaji wataalamu hawa uongozi wa Hospitali ya Mloganzila iliona ni vema kuunga mkono Idara ya tiba ya usingizi na ganzi kwa kuwapa fursa wataalam wake kupatiwa mafunzo.


Dkt. Muhochi ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Mloganzila kwa mafunzo haya na jinsi wataalam hao walivyokuwa na nidhamu katika kipindi chote cha mafunzo na kutoa wito kwa wataalam wengine wanaohudumia wagonjwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mafunzo ili kuongeza ujuzi.


Aidha Mratibu wa Mafunzo hayo Bw. Optatus Silanda ameishukuru hospitali kwa kusimamia mafunzo hadi kuhitimishwa kwake jambo ambalo limesaidia kuongeza idadi ya wataalamu hospitalini hapa ambao kupitia ujuzi walioupata watasidia kufundisha wataalamu wengine kutoa huduma hiyo kwa ufanisi.


Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Noel Kalinga amemshukuru Mungu, uongozi na waalimu kwa kipindi chote cha mafunzo hadi kuweza kuhitimu.