Wataalamu wa himofilia watakiwa kuwafikia wananchi wengi nchini

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya watoa huduma za afya kwa wagonjwa wa himofilia.

Baadhi ya wataalamu kutoka katika hospitali mbalimbali za wilaya na mikoa nchini wakiwa katika mafunzo hayo.

Bi. Happy Mambo (kulia) wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akimchoma sindano mmoja wa wagonjwa wa himofilia, Bw. Abdulsadiki Mgaza Mhina ikiwa ni sehemu ya tiba ya ugonjwa huo pamoja na kuwaonjesha washiriki wa mafunzo hayo jinsi sindano hiyo inavyochomwa.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Stella Rwezaura akiwasilisha mada kwa wagonjwa wa himofilia wakiwamo watoto.

Washiriki kutoka hospitali mbalimbali nchini wakifuatilia mafunzo hayo.

Watoto wenye himofilia wakiwa kwenye mkutano.

Baadhi ya watoto wakionekana wenye furaha wakati mada mbalimbali zikiendelea kutolewa kwenye mkutano huo.

Dkt. Stella Rwezaura (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo.


Na John Stephen

Wataalamu wa magonjwa ya damu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na wadau wengine wametakiwa kufikisha elimu ya ugonjwa wa himofilia kwa watu mbalimbali nchini ili waweze kufika kwenye vituo vya afya mapema kwa ajili ya matibabu endapo watapata maumivu au homa.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume wakati akifungua mafunzo ya Kuongeza Kasi ya Upatikanaji Huduma kwa Wagonjwa wa Damu (Selimundu na Himofilia) katika hospitali zote za rufaa nchini.

Novemba 18, 2020, Hospitali ya Taifa Muhimbili MNH) ilizindua mradi wa Kuongeza Kasi ya Upatikanaji Huduma kwa Wagonjwa wa Damu (Selimundu na Himofilia) kwa kushirikiana na wadau wa afya kama NNF na NNHF ili kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa wa Himofilia na Selimundu katika Hospitali zote za rufaa nchini, upatikanaji wa wataalamu wa afya waliobobea kwenye magonjwa haya pamoja na upatikanaji wa miundombinu sahihi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa pamoja na kuanzisha Kliniki za Himofilia na Selimundu kwenye Hospitali zote za rufaa na kutoa mafunzo elekezi kwa wataalamu wa afya nchini.

Dkt. Mfaume amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanafuatilia mafunzo hayo kwa makini ili waweze kuwahudumia wagonjwa wenye tatizo la Himofilia pamoja na kwenda kutoa elimu waliyoipata kwa wataalamu wengine.

Awali, wagonjwa wa Himofilia walipatiwa mafunzo jinsi ya  kujihudumia wakiwa nyumbani endapo wamepata maumivu au homa kabla ya kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya huduma za matibabu.

Pia, katika mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Stella Rwezaura aliwaeleza washiriki kwamba huduma ya matibabu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi ya damu ikiwemo Himofilia na Selimundu itaanza kutolewa katika hospitali za wilaya, mikoa, rufaa na kanda baada ya kukamilika kwa kliniki za kuwahudumia wagonjwa hao.

Amesema kwamba uanzishwaji wa kliniki hizo zitasaidia kuwafikia wagonjwa wengi na kwa wakati tofauti na sasa wanalazimika kufika Muhimbili kupata huduma hiyo.

“Tayari tumeshatembelea hospitali za mikoa na kanda ikiwemo Bugando, Benjamini Mkapa, KCMC na Mbeya ambako kliniki zinaendelea kujengwa,” amesema Dkt. Stella.

Daktari huyo amesema ili kufanikisha mpango huo wataalamu watapatiwa mafunzo ili kuwajengea uwezo wa kutoa huduma ya himofilia katika kliniki zilizoko katika ngazi ya wilaya na mikoa.

Akizungumzia kuhusu himofilia, amesema ni ukosefu wa chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu na kwamba ukosefu huo unasababisha damu kuvuja muda mrefu.

Amesema asilimia 97 ya wagonjwa wa himofilia hawajui kama wana ugonjwa huo na pia hawajawahi kupatiwa vipimo vyovyote ili kujua hali ya ugonjwa huo na hali hiyo imesababisha watu wengi kuhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina.

Katika hatua nyingine, Dkt. Stella amewashauri wananchi kufika hospitali mara moja pale wanapokuwa na viashiria vya kutokwa damu mfululizo na kwa muda mrefu au kupata mchubuko, kukatwa au kujikata.