Wataalamu 30 wahitimu mafunzo ya saratani ya matiti Mloganzila

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akizungumza na baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo yaliyolenga kuwajengea uwezo wataalam namna ya kufanya upasuaji wa saratani ya matiti kwa kutoa uvimbe bila kuondoa titi lote kwa wagonjwa wenye dalili za mwanzoni.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika hafla fupi ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa muda wa siku nne hospitalini hapa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage akitoa neno la shukrani wakati wa kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Matiti kutoka nchini Kenya, Dkt.Eric Hungu pamoja na timu ya wataalam bingwa wakishirikiana kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye titi bila kuharibu muonekano wa titi (Breast conserving surgery).

Baadhi ya washiriki wakiwa katika picha ya pamaoja mara baada ya kutunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo.


Na Dorcas David

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imehitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa mionzi na dawa jinsi ya kufanya upasuaji wa saratani ya matiti bila kuondoa au kukata titi la mgonjwa.

Akifunga Mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili  Prof. Lawrence Museru, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia  wataalamu hao kufanya upasuaji wa kutoa uvimbe kwa wagonjwa wenye saratani bila kutoa au kukata titi.

Dkt. Magandi amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri na kutoa elimu walioipata kwa wataalamu wenzao katika maeneo yao ya kazi.

"Mafunzo mliopata yasiishie hapa, hakikisheni huduma hii inakuwa endelevu kwa manufaa ya Watanzania.Tumieni elimu hii kuokoa maisha ya wagonjwa wa saratani ya matiti," amesema Dkt. Magandi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani  Ocean Road, Dkt. Julius Mwaisalage ameishukuru Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila na Kampuni hiyo ya dawa kwa mafunzo waliotoa kwa wataalamu hao kwani yatawawezesha kutoa huduma bora za kisasa kwa wagonjwa wa saratani ya matiti.

Mafunzo hayo yametolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kushirikiana na Kampuni ya Dawa ya Roche ya nchini Kenya.

Pia, mafunzo hayo yamewashirikisha wataalamu 30 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga & Mloganzila, Temeke, Amana, KCMC, Bugando, Dodoma, Mbeya,Ocean Road na Kenya.

Washiriki  wamepatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa muda wa siku nne na kutunukiwa vyeti.