Wataalam wabobezi Muhimbili Wapigwa msasa

Mkurugenzi wa Miradi Endelevu wa Shirika la Abbott, Dkt. Festo Kayandabila ambaye ni mmoja wa washiriki akieleza jinsi ya kupima malengo na namna ya kuyafuatilia ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Baadhi ya washiriki wa Muhimbili wakiwa kwenye mafunzo hayo leo.

Mtoa mada Macdonald Kiwia (kulia) akifafanua jambo baada ya kuwasilisha mada kuhusu namna bora ya kupima malengo na jinsi ya kufuatilia ili kuboresha huduma za afya Muhimbili.

Wataalam wabobezi wa Muhimbili wakifuatilia mada kuhusu namna bora ya kupima malengo.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inaendesha mafunzo ya siku tano kwa wahakiki na wasimamizi wa utoaji wa huduma bora (Quality Management Team) kwa lengo la kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa wanaofikishwa Muhimbili kupatiwa huduma za ubingwa wa juu.

Mafunzo yameanza Jumatatu wiki hii na yanatarajiwa kumalizika Mei 18, mwaka huu ambapo washiriki wamekuwa wakiibua hoja mabalimbali zikilenga jinsi wanavyotoa huduma kwa wagonjwa na namna gani wanaweza kuziboresha zaidi ili kupunguza rufaa za nje ya nchi.

Kabla ya mafunzo haya kutolewa, wataalam wabobezi wa Muhimbili wamekuwa wakitumia mifumo mbalimbali ya kupima na kufuatilia huduma za afya wanazozitoa kwa wagonjwa mbalimbali.

Katika mada ya leo, washiriki walijadili kwenye makundi mbalimbali na kufanya mazoezi ya jinsi ya kupima malengo na namna bora ya kufuatilia malengo hayo ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.

 Mmoja wa washiriki kutoka Kitengo cha Mapato, Bw. Clive Urima amesema leo wamekumbushwa kutekeleza na  kupima malengo ya Muhimbili pamoja na uanzishwaji wa huduma mpya za matibabu na kwamba kiashiria cha utekelezaji wa malengo hayo ni kutenga bajeti ya kuanzisha huduma mpya.

Naye Dkt Richard Christopher pamoja na wenzake wamejadiliana na kuongeza maarifa ya kupunguza rufaa za wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa kuzingatia utoaji wa huduma bora za ubingwa wa juu kupitia wataalam wabobezi.

Vilevile, Bi. Agnes Kabelege baada ya majadiliano wameongeza maarifa jinsi ya kufuatilia wagonjwa ana kwa ana ambao wanahitaji uangalizi maalum wodini.