Wataalam wa afya kutoka Japan watembelea Muhimbili

Wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na wataalam wa afya kutoka Japan wakijadiliana juu ya utoaji wa huduma bora za afya .

Mmoja wa wataalam kutoka Japan Yoshio Mikamo akielezea ambavyo huduma za afya zinatolewa nchini humo.

Wakurugenzi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wakisikiliza maelezo yanayotolewa na mtaalam huyo.

Mkuu wa Idara ya Famasia MNH Deus Buma akiwaelezea wataalam hao kuhusiana na huduma za utoaji dawa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mara baada ya kutembelea moja ya maduka ya dawa ya hospitali hiyo.

Meneja wa jengo la wagonjwa wa nje Sista June Samwel akifafanua huduma zinazotolewa katika jengo hilo.


Na Neema Wilson Mwangomo & Lightness Mndeme

Wataalam wa afya kutoka nchini Japan leo  wametembelea hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kufanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali hiyo.

Katika mazungumzo yao watalaam hao wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu  wa utoaji huduma za afya  na kujadiliana namna ambavyo wanaweza kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma .

Mkurugenzi wa huduma za tiba Dkt. Hedwiga Swai amesema MNH  ina mipango mbalimbali ya kuboresha huduma zake za ubingwa wa juu ikiwemo upandikizaji figo na kusisitiza kuwa huduma hiyo ni endelevu na imekuwa na mafanikio makubwa  tangu ilipoanzishwa kwa mara ya kwanza nchini Novemba mwaka jana  .

“Lengo letu ni kuhakikisha huduma za kibingwa zinakuwa endelevu lakini pia kama hospitali mipango yetu ni kuanzisha huduma zingine mpya ambazo hapo awali hazikuwepo”amesema Dkt. Swai.

Kwa upande Mkurugenzi wa huduma za tiba shirikishi Dkt. Praxeda Ogweyo amesema pamoja na mafanikio ambayo Muhimbili imepata lakini pia kuna changamoto ya upungufu wa watalaam katika  maeneo mbalimbali ya utoaji huduma .