Wataalam tarajali wasisitizwa nidhamu na uwajibikaji

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (kulia) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa madaktari na wauguzi tarajali, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Njoikiki Mapunda.

Baadhi ya wataalam wa afya walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo wakimsikiliza Naibu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi.

Daktari tarajali Tumaini Adolph akiuliza swali wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa wataalam tarajali katika Hospitali ya Mloganzila.


Na Lightness Mndeme

Wataalam tarajali wa fani mbalimbali za afya 80 walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wametakiwa kudumisha nidhamu na kujituma mahala pa kazi ili kujifunza na kupata ujuzi utakaowawezesha kutoa huduma bora za afya kwa watanzania.


Hayo yamesemwa leo na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi wakati akifungua mafunzo elekezi kwa wauguzi na madaktari tarajali na kuwasisitiza kufanya kazi kwa bidii pamoja na kufuata taratibu na miongozo iliyopo.


“Katika kipindi chote cha mwaka mmoja mtafanya kazi chini ya uangalizi wa wataalam wazoefu wa MNH-Mloganzila, kila mmoja hapa amekuja kujifunza ili kupata ujuzi hivyo nawasihi muwajibike katika majukumu mnayopangiwa kwa kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa na hospitali,” amesisitiza Dkt. Magandi.


Naye Daktari tarajali Tumaini Adolph amesema anajisikia vizuri kujiunga na mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Mloganzila na kwamba anaamini katika kipindi cha mwaka mmoja kitamsaidia kupata ujuzi utakaomuwezesha kutoa huduma stahiki kwa jamii inayomzunguka.