Wataalam nchini wajengewa uwezo kupunguza vifo kwa watoto

Mkuu wa Idara ya Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Marry Charles akizungumza katika Kongamano la siku mbili la kudhibiti maambukizi kwa watoto wachanga. Mkutano umefunguliwa na Dkt. Charles kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru.

Baadhi ya wataalam wa magonjwa ya watoto wachanga kutoka katika hospitali za Kanda, Rufaa, Wilaya na Mikoa wakiwamo wa MNH wakifuatilia kongamano hilo leo.

Dkt. Augustine Massawe akitoa mada kwenye kongamano hilo leo.

Baadhi ya wataalam wa magonjwa ya watoto wachanga wakifuatilia kongamano hilo leo.

Mtaalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto wachanga kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Naizihijwa Majani akitoa mada kwenye kongamano hilo leo.

Wataalam wamagonjwa ya watoto wakiwa katika picha ya pamoja katika ukumbi wa jengo la watoto. (Picha zote na John Stephen MNH)


Na Sophia Mtakasimba

Asilimia 25 ya vifo vya watoto wachanga  vinavyotokea nchini  vinawapata watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri wa kuzaliwa na wale wanaozaliwa wakiwa  na uzito chini kilo 1.8 kutokana na upungufu wa wataalamu wabobezi wa kuwatunza watoto hao, pamoja na ukosefu wa wodi maalumu zenye vifaatiba.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa Mshauri wa Magonjwa ya Watoto Wachanga Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Augustine Massawe wakati wa ufunguzi wa kongamano la pili la wataalamu wa magonjwa ya watoto linalofanyika MNH kwa ushirikiano wa Shirikisho la Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania (PAT).

“Mtoto anapozaliwa kabla ya kutimiza umri wake au akiwa na uzito mdogo anakuwa na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo kushindwa kunyonya, kushindwa kupumua vizuri na pia anaweza kuwa na shida ya figo kutofanya kazi vizuri, hivyo ili kutunza uhai wao inahitajika uangalizi wa karibu wa watalaamu wa afya, pamoja na uwepo wa wodi maalumu zenye vifaatiba maalumu vya kuwatunzia watoto hao.” amesema Dkt. Massawe.

Aidha, Dkt. Massawe amesema kuwa kwa kutambua changamoto hizo, MNH imejenga wodi maalumu kwa ajili ya watoto wachanga wenye changamoto mbalimbali  yenye vifaatiba vilivyojitosheleza ikiwemo vifaa vya kunawia mikono, mashine ya CPAP, mashine ya X-Ray na mashine ya kusaidia mtoto kupumua.
Dkt. Massawe ameeleza mbinu stahiki za kumsaidia mtoto mchanga anayezaliwa kabla ya muda ikiwemo kumpa  joto, kutunza kitovu  kisipate maambukizi, kuhakikisha  anapata maziwa na kuchunguza  dalili yoyote hatarishi.

Pia, amewataka wataalamu wa afya nchini wanaoshiriki kongamano hilo kuweka utaratibu wa kuendelea kujifunza zaidi kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Kongamano hilo  la siku mbili limefanyika katika kuadhimisha siku ya watoto waliozaliwa kabla ya muda wao  inayoadhimishwa Novemba 17 kila mwaka, linalenga kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi wanaohudumia watoto wachanga nchini kote ambalo limehudhuriwa na washiriki 150 kutoka hospitali za rufaa, kanda, wilaya na mikoa  mbalimbali ya Tanzania.

Mafunzo mbalimbali yanategemewa kutolewa ikiwemo  namna kuwahudumia watoto wachanga wanaopatwa na magonjwa mara baada ya kuzaliwa,  jinsi ya kudhibiti maambukizi, jinsi ya kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya muda wao na jinsi ya kumuhudumia mtoto aliyezaliwa na shida ya kupumua ili asipoteze maisha.