Wananchi washauriwa kutokata kidakatonge

Dkt. Abdallah Omari akitoa elimu juu ya magomjwa ya figo kwa watu mbalimbali waliotembela Banda la Hospitali ya Muhimbili Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila katika viwanja vya Sabasaba.

Afisa Muuguzi Petro Mathias kutoka Muhimbili-Mloganzila akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kutokata kidaka tonge ili kuepuka madhara mbalimbali yanayoweza kujitokeza.

Daktari wa meno, Christopher Rweihimba akimpatia matibabu Bw. Budeba Mlyaketo alipofika kwenye Banda la Muhimbili.

Daktari Bingwa wa macho kutoka Muhimbili-Mloganzila Dkt. Catherine Makunja akitoa huduma ya matibabu ya macho kwa mtoto Nuru Lwamo alipofika kwenye Banda la Muhimbili lilopo viwanja vya Sabasaba.

Afisa Muuguzi Daudi Mapunda kutoka Muhimbili- Upanga akitoa elimu kwa Anjela Kajitanus juu ya namna wanamhudumia mtoto anayehitaji uangalizi maalum katika viwanja vya Sabasaba.


Na Priscus Silayo

Wananchi wameshauriwa kuacha tabia ya kukata kimeo (kidaka tonge) kwa kuwa kunaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi na hatimaye kusababisha kifo kwa mhusika.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Bw. Petro Mathias katika maonesho ya 45 ya biashara yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam.

Bw. Mathias amesema mtu anapohisi kidaka tonge chake kimeongezeka ukubwa afike kituo cha kutolea huduma kilichokaribu nayeye aweze kupata matibabu baladala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji au kukikata.

Amesema kazi ya kidaka tonge ni kukinga chakula kisiingie kwenye njia ya hewa na kumsababishia mtu kukohoa na kupaliwa, hivyo kikikatwa kinaathiri kazi yake ya kawaida.

“Kidaka tonge kikiwa na afya njema hakigusi kuta za njia ya hewa ila kikipata maambukizi ya wadudu hususani bakteria huvimba na kuongezeka ukubwa na kugusa njia ya hewa na kusababisha mtu kukereketwa na kukohoa, kukohoa ni namna ya kusababisha njia ya hewa” amesema Bw. Mathias

Bw. Mohamed Abdallah aliyefika kupata huduma amesema anajua kuwa kidakatonge huwa kinakuwa kirefu na kuhitaji kukatwa na hivyo elimu aliyoipata atawasaidia  watu wengine ili waache tabia ya kukata vidaka tonge kwakuwa ni kinyume na ushauri wa kitaalam.

Naye, Bw. Shabani Simba kutoka Rufiji amesema amefurahishwa na kunufaika na elimu inayotolewa na Hospitali ya Muhimbili ikiwemo ya kutoa mawe kwenye figo kwa kutumia mashine maalum bila kufanya upasuaji.

Adha, wananchi wamewapongeza wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila)  kwa ukarimu wao katika kutoa elimu na matibabu kwa wananchi wanaofika katika banda hilo.

Wanachi mbalimbali wamejitokeza kwenye Banda la Muhimbili kupata huduma ya meno, macho, huduma za dharura, ushauri kuhusu lishe na mtindo bora wa maisha na elimu kuhusu magonjwa ya figo.