Wananchi wamiminika Mloganzila kupima usikivu

Daktari Bingwa wa Upasuaji Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo, Dkt. Godlove Mfuko wa Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila akimpima mgonjwa kiwango cha usikivu katika zoezi la upimaji wa usikivu linalofanyika leo hospitalini hapo leo na kesho.

Katika picha baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima kiwango cha usikivu hospitalini hapo.

Wazazi wakiwa na watoto kabla ya kwenda kuwaona wataalam wa magonjwa ya masikio, pua na koo wa Hospitali ya Muhimbili Upanga na Mloganzila.

Wananchi wakisubiri kupata huduma ya upimaji ya usikivu katika Hospitali ya Mloganzila.

Mratibu wa Usikivu kutoka Mfuko wa Usikivu wa Starkey akitoa elimu kwa wananchi wanaosubiri kuwaona wataalam wa magonjwa ya masikio, pua na koo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

Mtaalam wa magonjwa ya masikio, pua na koo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Teddy Uisso akimpima mgonjwa kiwango cha kusikia.

Wananchi wakisubiri kupata huduma kutoka kwa wataalam wa magonjwa ya masikio, pua na koo katika Hospitali ya Muhimbili Upanga na Mloganzila.


Na Abubakary Mahamoud Omary

Wingi wa watu waliojitokeza leo kupima usikivu wao umeonyesha ni jinsi gani wananchi wanajali afya zao, huku wakipewa sababu zinazosababisha baadhi ya watu kupoteza uwezo wa kusikia na jinsi ya kuzuia upotevu wa kusikia.
Upimaji wa usikivu bila malipo umeanza leo Machi 2, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ambapo kauli mbiu ni "Chunguza Usikivu Wako (Check Your Hearing” yenye lengo la kuhamasisha kila mmoja kuchukua hatua ya kufanyiwa uchunguzi wa usikivu wake.
Huduma ambazo zimeanza kutolewa leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ni; upimaji wa kuona kiwango cha kusikia na rufaa ya kupata matibabu Muhimbili kwa watakaobainika kuwa na tatizo. Pia elimu ambayo imetolewa ni dalili na vyanzo vya kupoteza usikivu, kutoa takwimu za ongezeko la upotevu wa usikivu duniani na hatua zinazochukuliwa nchini.
Katika shughuli ya upimaji huo, wananchi wameelezwa sababu zinazosababisha mtu au watu kupoteza uwezo wa kusikia. Zifuatazo ni sababu zinazosababisha watoto wachanga kupoteza uwezo wa kusikia. Kwanza familia kuwa na watu wenye matatizo ya kutokusikia, maambukizi ya magonjwa kutoka kwa mama wakati akiwa mjamzito, mtoto kuzaliwa kabla ya wakati, mtoto kukosa hewa wakati wa kuzaliwa na kupata homa ya manjano baada ya kuzaliwa.
Kwa upande wa watoto na watu wazima, sababu zinazosababisha kupoteza uwezo wa kusikia ni; kuugua surua, uti wa mgongo au sikio kupata maambukizi na uchafu kutoka sikioni, matumizi yasiyo sahihi ya dawa mbalimbali, kuumia sikio au kichwa, kukaa sehemu zenye kelele au zenye sauti kubwa sana, kusikiliza sauti kupitia vifaa mbalimbali kabla ya umri unaofaa na nta au kitu kisichokuwa cha kawaida kuziba mfumo wa njia ya sikio.

Wazee nao wamekuwa wakipoteza uwezo wa kusikia kutokana umri wao hivyo uwezo wao wa kusikia hupungua, kukaa sehemu zenye kelele au zenye sauti kubwa sana, kupata shinikizo la damu, kuugua sukari na wengine kutumia dawa mbalimbali.

Wataalam wa magonjwa ya masikio, pua na koo wanaeleza kuwa njia za kuzuia upotevu wa kusikia kwa mtu mzima ni kuweka kifaa au kitu chochote ndani ya sikio, anashauriwa kutumia pamba laini au kifaa maalumu cha kuziba masikio kwenye sehemu zenye sauti kubwa, endapo ana shida ya sikio au masikio anatakiwa kumuona daktari, anatakiwa kuchunguza dawa anazotumia kama zinaweza kuathiri usikivu wake na pia, anashauriwa kutumia vifaa salama vya masikio kama ulivyoelekezwa na daktari.

Kwa upande wa watoto; mzazi anashauriwa asimweke mtoto kifaa au kitu chochote ndani ya sikio labda kama unamsafisha sikio, watoto wanapaswa kufundishwa kutokuweka kifaa au kitu chochote ndani ya sikio, endapo  sikio la mtoto linauma, limeumia, kukatika au linatoka uchafu  ndani mpeleke kwa daktari, usiwaruhusu watoto kuogelea kwenye maji machafu, mzazi usimpige mtoto sehemu za sikio, mkinge mtoto katika sehemu zenye sauti au kelele kubwa na wafundishe watoto kusikiliza kwa kutumia vifaa salama.

Katika hatua hii, mzazi au mlezi anawezaje kuhisi mtoto wake amepoteza uwezo wa kusikia? Mtoto anaweza kuwa na matatizo ya kutokusikia ikiwa hatojibu jambo kwa sauti, kutokuelewa kitu gani kinazungumzwa au kushindwa kuongea kwa ufasaha, kuchelewa kuongea kwa ufasaha, kutokwa na uchafu sikioni, na kuumwa sikio mara kwa mara au sikio kuziba.
Kwa upande wa mtu mzima atakuwa amepoteza uwezo wa kusikia endapo;  atauliza mara kwa mara watu warudie walichoongea, kuwa na tabia ya kuongeza sauti ya redio na runinga, kukosa baadhi ya maneno katika maongezi, kuwa na kelele katika sikio na wakati mwingine watu wanakwambia unaongea kwa sauti kubwa sana.

Upimaji wa usikivu bila malipo umeanza leo Machi 02,2019 na utamalizika Kesho Machi 03,2019.