WANANCHI 2,360 WATEMBELEA BANDA LA MUHIMBILI-1,220 WAHUDUMIWA, WANAUME 18 WACHUNGUZWA SARATANI YA MATITI

Mke wa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa akipata huduma ya macho kutoka kwa mtaalamu wa optometria Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Bi. Elizabeth Mahende kwenye maonyesho ya Sabasaba 2020.

Baadhi wa Wananchi wakisubiri kupata huduma katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) katika maonyesho ya Sabasaba 2020.

Baadhi ya wananchi wakisubiri kupima saratani ya matiti baada ya kupata elimu kwenye maonyesho ya Sabasaba 2020.

Wananchi wakipata elimu kuhusu namna Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inavyowahudumia wagonjwa katika Idara ya Magonjwa ya Dharura.


Na Sophia Mtakasimba

 

Jumla ya wananchi 2,360 wametembelea banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili kwenye maonesho ya 44 ya biashara SABASABA tangu Julai Mosi hadi Julai 07, mwaka huu.

Wananchi 1,220  wamepata huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia kliniki ya uchunguzi wa macho, saratani ya matiti na huduma za  dharura.

Kwa upande wa huduma za macho wananchi 634 wamehudumiwa ambapo kati yao 52 wamegundulika kuwa na matatizo ya macho yanayohitaji uchunguzi zaidi hivyo kupewa rufaa moja kwa moja kwenda Muhimbili huku 105 wamepatiwa miwani ya kusomea.

Wananchi 235  wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti, kati ya hao 11 walionekana kuwa na viashiria vya saratani hivyo wamepatiwa rufaa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Katika idadi hiyo wanaume 18 nao wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na kukutwa hawana viashiria vya ugonjwa huo.

Waliohudumiwa kupitia kliniki ya magonjwa ya dharura ni 351 ambapo 37 wamekutwa na matatizo mbalimbali na kupatiwa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi kupitia Hospitali za Muhimbili zilizopo Upanga na Mloganzila.

Huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti, dharura  pamoja na macho zinazotolewa bila malipo isipokua kwa wale wanaogundulika kuwa na matatizo ya kusoma wanapewa miwani kwa kuchangia TZS. 10,000 tu.

Kwa upande mwingine, wananchi wote waliotembelea banda la Muhimbili walipata nafasi ya kufahamu juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Hospitali zetu zikiwemo huduma za kibingwa na bobezi.

Hospitali ya Taifa Muhimbili inawahimiza wananchi kujitokeza kutumia fursa hii ya sabasaba kupata huduma zinazotolewa hadi Julai 13, 2020 ambapo maonesho yatafungwa rasmi.