‘Wafanyakazi wapya msiwanyanyase wagonjwa, tumieni lugha nzuri'

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bw. Yassin Munguatosha akizungumza na wafanyakazi wapya kuhusu kuzingatia maadili.

Baadhi ya wafanyakazi wakifuatilia maelekezo kutoka kwa mwenyekiti wa kamati.

Mratibu wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Matibabu wa Muhimbili, Bi. Niyonizigiye Anicet akitoa mafunzo elekezi kwa wafanyakazi wapya.

Wafanyakazi wapya, wafanyakazi wa kujitolea na wanafunzi tarajali kutoka TAESA.

Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Ajira wa MNH, Bw. Abdallah Chiwanga akitoa mada katika mafunzo hayo.

Mafunzo elekezi yakiendelea.

Bi. Elizabeth Fupe akitoa mada katika mafunzo hayo.


Na John Stephen

Kamati ya Maadili, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imewataka waajiriwa wapya kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa, kutojihusisha na vitendo vya unyanyasaji na daima  wameshauriwa kutumia lugha nzuri wakati wa kutoa huduma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Muhimbili, Bw. Yassin Munguatosha wakati wa mafunzo elekezi  kwa wafanyakazi wapya, wafanyakazi wa kujitolea na wanafunzi tarajali kutoka TAESA pamoja na kuwapatia miongozi mbalimbali ya utendaji kazi.

Bw. Munguatosha amewataka kuzingatia taratibu za utoaji wa huduma kwa wagonjwa kwa kuwa kazi ya kamati hiyo ni kuwalinda wagonjwa na pia kudhibiti viashiria hatarishi ambavyo vinaweza kusababisha hasara au kuharibu sura ya hospitali.

Amesema endapo kamati itagundua wanakwenda kinyume na taratibu za kazi watachukuliwa hatua za kinidhamu ili kulinda haki za wagonjwa pamoja na kuendelea kutoa huduma bora za matibabu.

“Hakikisheni mnazingatia maadili ya kazi na msijihusishe katika vitendo vya rushwa,” amesema Bw. Munguatosha.

Naye Mratibu wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Matibabu wa Muhimbili, Bi. Niyonizigiye Anicet amewataka wafanyakazi wapya, wafanyakazi wa kujitolea na wanafunzi tarajali kusikiliza maoni ya wagonjwa ili hospitali iweze kuboresha huduma za matibabu.

“Kazi yenu kubwa ni kutoa matibabu kwa wagonjwa lakini pia msisahau kuwaeleza jinsi wanavyopaswa kutibiwa, wapatieni mtiririko mzima wa matibabu,” amesema Bi.  Niyonizigiye.