Wafanyakazi Muhimbili watoa msaada kwa wagonjwa

Kushoto ni Paroko wa Kanisa Katoliki Muhimbili, Padri Herbert Mrosso, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru na viongozi wengine wakisikiliza risala kutoka Bi. Cresensia wa Chama cha kitume cha Wafanyakazi Wakatoliki wa Muhimbili.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho.

Mmoja wa wanachama wa chama hicho, Bi. Cresensia akisoma risala kwa Prof. Museru ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Meneja wa Jengo la Kibasila, Bi. Haika Ngozi akipokea baadhi ya msaada kutoka kwa Bi. Jenifer Msoma kwa ajili ya kuwakabidhi wagonjwa wa jengo hilo.

Wataalamu wa afya wakiwa katika picha ya pamoja.


Na Sophia Mtakasimba

Chama cha kitume cha Wafanyakazi Wakatoliki wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi taasisi zilizopo muhimbili Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye taasisi hizo ikiwa ni kutekeleza moja ya jukumu lake la kutoa huduma za matendo ya huruma kwa wahitaji.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema Muhimbili na taasisi zilizopo Muhimbili zina wagonjwa 1,800 kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao wamelazwa wodini.

Amesema kutokana na matibabu kuchukua muda mrefu, ana imani kwamba kikundi hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa kwa sababu mahitaji yao yamekuwa yakiongezeka.

“Mgonjwa anapokaa wodini muda mrefu hata mahitaji yao huongezeka, Serikali na hospitali peke yake haziwezi kukidhi hayo yote, hivyo naamini kikundi hiki kitasaidia sana wagonjwa wenye mahitaji maalumu,” amesema Prof. Museru.

Prof. Museru ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa chama hicho ili kiweze kutimiza majukumu yake.

Naye, Paroko wa Kanisa Katoliki Muhimbili Padri Herbert Mrosso amemshukuru Prof. Museru kwa kukubali kushiriki kwenye tukio hilo kwani jambo hilo linaashiria chama hicho kimepokelewa vizuri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho Bi. Praxeda Chenya amesema mbali ya kufanya matendo ya huruma chama hicho kina majukumu mengine ambayo ni pamoja na kwezesha wafanyakazi ambao wanakosa fursa za huduma za kiroho katika parokia hiyo kupata huduma kwenye Parokia ya Muhimbili, kujenga umoja na mshikamano kwa wafanyakazi na kuwalea kimaadili watumishi katika maeneo yao ya kazi.