WAFANYAKAZI MUHIMBILI WAHIMIZWA KUCHUNGUZWA HOMA YA INI

Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. John Rwegasha akiwasilisha mada kuhusu upimaji, chanjo na matibabu ya homa ya ini (hepatitis B) kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili.

Baadhi ya wafanyakazi wa MNH wakifuatilia kongamano hili linalofanyika hospitalini hapa leo.

Wafanyakazi wakifuatilia kwa makini jinsi ya kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa wa homa ya ini na hatua wanazopaswa kufuata ili kupima afya zao.

Mmoja wa wafanyakazi wa MNH, William Musiba akiuliza swali ili kupata ufafanuzi juu ya mada iliyotolewa na Dkt. Rwegasha leo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula wa Muhimbili, Dkt. Masolwa Ng’wanasai akifafanua jambo kwenye kongamano hili leo.

Baadhi ya wafanyakazi wakifuatilia kongamano hili leo.

Kongamano hili limewakutanisha wataalam mbalimbali wa Muhimbili kama inavyoonekana kwenye picha.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Muhimbili, Dkt. Hedwiga Swai akiwahimiza wafanyakazi kupima afya zao ili kubaini kama wamepata homa ya ini na hivyo kuanza matibabu mapema.


Na John Stephen

Wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hususani wale wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi wameimizwa kufanya uchunguzi wa homa ya ini ili watakaobainika kuwa na tatizo hilo wapewe tiba kulingana na miongozo ya tiba inavyoelekeza.

Hayo yamesemwa leo na Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Tumbo, Dkt. John Rwegasha wakati akiwasilisha mada kwenye Kongamano la Kisayansi linalofanyika kila Alhamisi hospitalini hapa ambapo mada ilikua ni upimaji, chanjo na matibabu ya homa ya ini (hepatitis B.

Ugonjwa wa Homa ya Ini (Hepatitis B) ni nini

Ugonjwa wa homa ya Ini (Hepatitis) unasababishwa na virusi viitwavyo “Hepatitis B na C” na maambukizi ya ugonjwa huu yanashabiana na njia ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kama vile kufanya ngono zisizo salama, kuchangia sindano au vikatio, kupewa damu isiyo pimwa, kupitia uzazi wa mama na mtoto hasa wakati wa kujifungua.

Akizungumza na mamia ya wafanyakazi waliohudhuria kongamano hilo Dkt. Rwegasha amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa watu nane kati ya watu mia moja wana maambukizi ya ugonjwa huu hivyo ni muhimu kuchukua hatua.

Tiba

Kama ilivyo kwa ugonjwa wa ukimwi, ugonjwa huu sugu wa homa ya ini hauna tiba ya kuponya, isipokuwa dawa zilizo patikana hadi sasa zinaweza kupunguza kasi ya maambukizi mwilini na kuzuia madhara zaidi kwenye ini.

“Mgonjwa yeyote aliyepatikana na ugonjwa huu, inabidi kutumia dawa hizi kwa muda mrefu usiopungua miaka mitano ili kuweza kufanikisha lengo hili ikiwa ni pamoja na kumwezesha mgonjwa kufikia hatua ya kujitengenezea kinga ya mwili inayohitajika kuweza kuudhibiti ugonjwa huu mwilini,” amesema Dkt. Rwegasha.

Dalili

Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu na kusababisha maradhi mwilini pasipo kuwa na dalili za aina yoyote ingawa kuna baadhi ya waathirika hupata dalili kama vile njano ya macho, tumbo kuuma, kichefuchefu, kutapika na kuharisha kwa muda mfupi, mwili kuwashwa, au kupata mkojo wa njano nyingi.

 

Wito Wetu

Tunapenda kuwafahamisha wananchi kupitia fursa hii kwamba wote walioathirika na tatizo hili wajitokeze kwa wingi ili waweze  kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupata  nafasi ya tiba  kulingana  na miongozo inavyoelekeza.