Wachezaji wa Simba wampa faraja mtoto Bakari Muhimbili

Daktari wa Watoto, Dkt. Karim Bembe, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na viongozi wa Simba kuhusu afya ya mtoto Bakari Juma Selemani ambaye amelazwa katika wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu kutokana na kuugua maradhi ya kupooza misuli.

Pichani Pape Sakho mmoja wachezaji ambao Bakari alitaka kuwaona.

Aishi Manula akimtakia heri Bakari ili apate nafuu na kuweza kuendelea na maisha yake ya kawaida.


Na John Stephen

 

Mtoto Bakari Juma Selemani ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ametembelewa na viongozi na wachezaji wa Simba ‘wekundu wa Mzimbazi’ ili kumjulia hali kutokana na kuugua maradhi ya kupooza misuli.

Bakari aliletwa Muhimbili Desemba mwaka jana, akitokea Hospitali ya Rufaa Temeke kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi na baada ya afya yake kuimarika alionyesha mapenzi yake kwa timu ya Simba.

Kabla ya kufika kwa wachezaji hao, Bakari alionyesha shauku kubwa ya kutaka kuwaona wachezaji wa timu hiyo, akiwamo Aishi Manula, Jonas Mkude, Larry Bwalya, Pape Sakho na Cloutus Chama, lakini pia aliwaona wachezaji wengine na viongozi wa timu hiyo, Barbra Gonzalez na kocha Pablo.

Akizungumza na wachezaji wa Simba, Dkt. Karimu Bembe amesema  afya ya Bakari inaendelea kuimarika kutokana na matibabu anayopatiwa na wataalamu wa wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (PICU).

“Bakari ni shabiki mkubwa wa Simba, anaipenda Simba, ukimwambia kuwa tutakupa jezi ya Simba anatoa ushirikiano mkubwa, huku tukiendelea kumpatia matibabu,” amesema Dkt. Karimu.

Naye, Msemaji wa Timu ya Simba, Bw. Ahmed Ally amesema wamefika Muhimbili kumpa faraja Bakari baada ya kusikia ugonjwa wake na mapenzi yake juu ya Simba.

“Tulipata taarifa juu ya Bakari kwamba kiu yake kubwa ni kuwaomba wachenzaji wa Simba, leo tumekuja Muhimbili kumuona, tumekuja kumjulia hali, lakini kumtia moyo katika kipindi hiki anachopambania afya yake,” amesema Bw. Ally.