Viongozi Muhimbili wapigwa msasa

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Makwaia Makani akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi yaliyohusisha viongozi wa Muhimbili Upanga na Mloganzila.

Viongozi wa Muhimbili Upanga na Mloganzila wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo leo.

Muwezeshaji wa mafunzo ya uongozi Bw. Ntangeki Nshala akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya uongozi wakifuatilia mada kusuhu misingi ya uongozi na utawala, mafunzo hayo yametolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili .


Na Neema Wilson Mwangomo

 

Viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wametakiwa  kufanya kazi kwa bidii ili kuwa mfano bora wa kuigwa na watendaji wa chini wanaowaongoza .

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Makwaia Makani wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru, mafunzo hayo yamehusisha viongozi wa Muhimbili Upanga na Mloganzila.

Bw. Makani amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha viongozi katika utendaji wao wa kazi wa kila siku ili kufikia malengo na kwamba Muhimbili imejiwekea utaratibu wa kutoa mafunzo haya kila mwaka .

“Huu ni utaratibu wa kawaida ambao Hospitali ya Taifa Muhimbili tumejiwekea kwa kila mwaka kutoa mafunzo kwa viongozi wakiwemo wakurugenzi, wakuu wa idara pamoja na wakuu wa vitengo, pia mafunzo haya ambayo yameanza leo na yatahitimishwa kesho yamehusisha viongozi wapya wa Muhimbili-Mloganzila ambao waliteuliwa mara baada ya MNH kukabidhiwa kuisimamia Hospitali ya Mloganzila’’ amesema Bw. Makani.

Katika mafunzo hayo ya siku mbili jumla ya mada kadhaa zitawasilishwa ikiwemo misingi uongozi , namna ya kuongoza timu ,misingi ya mawasiliano na makosa yaliyozoeleka katika uongozi.