Ubunifu wapunguza gharama za ununuzi wa dawa Muhimbili

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila, Prof. Lawrence Museru akizungumza na wafamasia wa MNH ambao wamekutana kuadhimisha wiki ya famasi ambayo imefanyika katika viwanja vya Muhimbili Upanga na Mloganzila.

Wafamasia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga wakimsikiliza Prof. Museru.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Famasi Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Bw. Paul Mayengo akitoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma.

Mfamasia Marcus Johansen kutoka Mloganzila akitoa mada juu namna bora ya utunzaji wa dawa kwa matumizi ya binadamu.

Bw. Mariki Ibrahim ambaye ni mfamasia kutoka Mloganzila akiwasisitiza wananchi kuacha tabia ya kununua dawa bila kupata ushauri wa daktari.

Mkuu wa Idara ya Famasi, Muhimbili Upanga akizungumza katika mkutano na wafamasia wa MNH-Upanga.

Baadhi ya wafamasia wa Muhimbili Upanga wakiwa kwenye mkutano huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Upanga na Mloganzila, Prof. Museru akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafamasia wa Muhimbili Upanga.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafamasia wa Hospitali ya Mloganzila baada ya maadhimisho hayo.


Na Priscus Silayo

Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila imesema mfumo uliobuniwa na wafamasia kutoa dawa kwa wagonjwa umesaidia kupunguza gharama za ununuzi wa dawa katika hospitali hizo sambamba na wananchi wameshauriwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu hao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Upanga na Mloganzila, Prof. Lawrence Museru wakati akizungumza na wafamasia kwenye maadhimisho ya wiki ya famasi ambayo imefanyika katika viwanja vya Muhimbili Upanga na Mloganzila.

“Kitu ambacho tumekikazania ni matumizi bora na matumizi sahihi ya dawa, jambo hili linazingatiwa na wafamasia wa MNH Upanga na Mloganzila,” amesema Prof. Museru.

Amesema kutokana na mfumo huo, wagonjwa waliolazwa wodini wamekuwa wakipewa dawa za siku ili kuepuka gharama na vile vile mfumo huo unalenga kuwasaidia madaktari kubadilisha dawa endapo  zitahitajika kufanya hivyo.

Akizungumzia ujenzi wa kutengeneza dawa za maji (infusion unit), Prof. Museru aliishukuru Serikali kwa kutoa kiasi cha Tzs. 2 bilioni kwa ajili ya kutengeneza kiwanda cha tiba maji na kwamba Muhimbili Upanga na Mloganzila itashirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha ujenzi huo haraka.

Mkuu wa Idara ya Famasi, Muhimbili Upanga, Dkt. Deus Buma alisema madhumuni ya maadhimisho hayo ni  kuikumbusha jamii, kuhusu matumizi sahihi ya dawa na madhara ya kutumia dawa bila maelekezo ya daktari.

“Hapa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wafamasia tutaendelea kuhakikisha dawa zinapatikana kwa kushirikiana na viongozi wetu sambamba na hili, tutaendelea kusimamia matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba,” amesema Dkt. Buma.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Famasi, Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila, Bw. Paul Mayengo akizungumzia kuhusu matumizi sahihi, alisema kuwa dawa ikitumika vibaya kuna uwezekano mkubwa wa dawa kutomsaidia mgonjwa na kupelekea kupata madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na figo kushindwa kufanya kazi ipasavyo, kuharibu ini, mapigo ya moyo kwenda kwa kasi na kuleta athari katika mfumo wa upumuaji.

“Matumizi sahihi ya dawa ni pamoja na kuzingatia muda wa kutumia dawa, kama umeambiwa utumie dawa mara tatu kwa siku maana yake unachukua saa 24 unagawa kwa tatu ambapo utapata ni saa nane hivyo utajua utumie dawa hiyo muda gani kwa kuzingatia saa nane,” amesema Bw. Mayengo.

Pia, Mfamasia Thomas Lukuba ameshauri wananchi kuacha tabia ya kuchanganya dawa na pombe kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri ubora wa dawa na wakati mwingine dawa kugeuka kuwa sumu.

Kwa upande wake, Mfamasia Marcus Johansen amesema dawa inatakiwa itunzwe katika mazingira ambayo hayana jua na kavu kwa kuweka katika maeneo yenye jua au unyevunyevu yanaweza kusababisha dawa kupoteza ubora na hivyo kushindwa kumsaidia mgonjwa kupona maradhi yanayo mkabili.

Aiha, Mfamasia Mariki Ibrahim amewashauri wananchi kuacha tabia ya kununua dawa kwenye maduka mbalimbali bila kupata ushauri wa daktari.

Siku ya famasia nchini huazimishwa kila mwaka Juni 16, na mwaka huu kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Timu madhubuti: Hufanya kazi na wafamasia kuboresha huduma kwa wagonjwa’.