Tuna imani kubwa na madaktari wa Muhimbili: Prof. Museru

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na madaktari, wafamasia, wataalamu wa Tehama pamoja na wataalamu wengine kuhusu changamoto katika maeneo yao ya kazi.

Baadhi ya madaktari na wafamasia wakimsikiliza Prof. Museru pamoja na wakurugenzi wengine (pichani hawamo) kuhusu jinsi menejimenti ya hospitali itakavyotatua changamoto walizoeleza kwenye kikakao hicho.

Madaktari wa kada mbalimbali wa Muhimbili wakieleza changamoto katika maeneo yao ya kazi kwa menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Muhimbili, Bw. Gerald Jeremiah akiwa katika kikao hicho.


Na Priscus Silayo

 

Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umesema una imani kubwa na madaktari wa hospitali hiyo pamoja na wataalamu wengine kutokana na utendaji kazi wao wa kila siku.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru wakati akizungumza na wataalamu wa afya wakiwamo madaktari, wafamasia na wataalamu wengine wa hospitali katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo hufanyika kila mwaka Juni kuanzia tarehe 16 hadi 23.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata katika mazingira ya migogoro.”

Hospitali  imeadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa utaratibu wa Menejimenti kukutana na wafanyakazi kupitia makundi mbalimbali ya kada zao za afya ili kupokea kero, malalamiko wanazopatiwa wakati wa utoaji huduma.

Katika kikao hicho, madaktari na watalaamu wengine wa hospitali walieleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maeneo ya kazi na hivyo kuomba uongozi wa hospitali kutatua changamoto ya mfumo mawasiliano wa Tehama kuanzia katika hatua ya kusajili wagonjwa hadi kumfikia daktari.

Pia, wataalamu hao wameomba kujengewa ofisi kwa kuwa zilizopo hazitoshelezi mahitaji ya wataalamu hao.

Katika kikao hicho, vilevile watalaamu walieleza kuwapo kwa ukosefu wa baadhi ya dawa, huku uongozi wa hospitali ukiahidi kufanyia kazi changamoto zilizowasilishwa kwenye kikao hicho.

Akizungumzia changamoto hizo, Prof. Museru amesema Uongozi wa hospitali utanunua vifaa tiba vipya kulingangana  na upatikanaji wa fedha na pia itanunua mashine ambazo zitatumika endapo itatokea tatizo la baadhi ya  mashine kutokufanya kazi.

Pia, Prof. Museru ameahidi kuboresha mfumo wa mawasiliano wa Tehama na kwamba kila mtumishi  katika Hospitali ya Muhimbili atimize wajibu wake ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Aliwaeleza wataalamu hao kwamba hospitali itaendelea kupanua wigo wa kliniki ili ziendelee hadi usiku na zifanyike siku za wikiendi ili kuondoa msongamano wa wagonjwa nyakati za asubuhi.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Muhimbili, Dkt. Hedwiga Swai amesema hospitali inaendelea kushughulikia upatikanaji wa dawa ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana.

“Ni kweli kulikuwa na changamoto ya ukosefu wa baadhi ya dawa kutokakana na janga la ugonjwa wa COVID-19 kwani baadhi ya nchi zilifunga mipaka yao na mawasiliano ya usafiri kuwa magumu...pamoja hilo tunaendelea kutatua tatizo hili,” amesema.