TUGHE Mloganzila watakiwa kudumisha nidhamu na ushirikiano

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na wanachama wa TUGHE tawi la Muhimbili-Mloganzila kabla ya kufungua rasmi mkutano. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi na kulia ni Mwenyekiti wa TUGHE, Bw. Amon Chizua akifuatiwa na Kaimu Katibu wa TUGHE Bw. Jumanne Mwalimu.

Baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo uliofanyika Mloganzila.

Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Muhimbili-Mloganzila, Bw. Amon Chizua akielezea mafanikio mbalimbali yaliyopatika tangu kuanzishwa kwa tawi hilo mwaka 2018.

Baadhi ya viongozi wa TUGHE na wanachama wakiwa katika picha ya pamoja.

Baadhi ya wanachama wakiimba wimbo wa mshikamano mara baada ya mkutano.


Na Dorcas David

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Sekta ya Afya (TUGHE) Tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila kimefanya mkutano wake wa kwanza ambao umejadili mambo mbalimbali ya ikiwemo kufanya uchaguzi wa viongozi watakaoziba nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.

Sababu hizo ni pamoja na vifo, kuhama kwa baadhi ya viongozi pamoja kustaafu Utumishi wa Umma ambapo nafasi zilizoathirika ni pamoja na katibu wa tawi, mwenyekiti kamati ya wanawake na wajumbe watatu wa halmashauri ya tawi.

Waliochaguliwa ni pamoja na Dkt Peter Kibacha (Katibu), Sis. Twitike Kalinga (Mwenyekiti kamati ya wanawake) na wajumbe watatu wa halmashauri kuu ambao ni Bw. David Kivamba, Bi Elizabeth Jonathan na Bw.Amos Bukelebe. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru ambaye pia ni mgeni rasmi wa mkutano huo amewataka wanachama kudumisha ushirikiano na nidhamu ndani ya chama.

Prof. Museru amesema nidhamu itasaidia kuliimarisha tawi kwa umoja kwani kila mwanachama atafanya kazi kwa kuzingatia mipaka yake na kutoathiri utendaji ndani ya tawi.

Amefafanua kuwa uongozi wa hospitali unafanya kazi kwa ukaribu  na TUGHE kitu ambacho kimesaidia kuwepo kwa utulivu mahali pa kazi muda wote kwakuwa changamoto zinajadiliwa kwa pamoja na kupata ufumbuzi.

 “Uongozi wa Muhimbili unajivunia ushirikiano na uhusiano ulipo baina yake na TUGHE ambao umesaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza mahala pa kazi na kupata majawabu ya changamoto hizo kwa ustawi wa pande zote mbili” amesema Prof. Museru.

Kwa upande mwingine amewataka viongozi kuendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wafanyakazi wa Mloganzila kujiunga kwa wingi na chama hicho kwa kuwa nguvu ya tawi pamoja na mambo mengine inapimwa na idadi ya wanachama hai waliopo.

Akielezea mafanikio ya chama mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mloganzila Bw. Yona Chizua amesema chama kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama kutoka 20 mpaka 131, na kufanikisha kupatiwa ofisi rasmi ya chama. 

Ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja kufungua akaunti rasmi ya chama kwa ajili ya mapato ya chama, kufanikisha mchakato wa uundwaji wa mkataba wa baraza la wafanyakazi la MNH-Mloganzila, kuundwa kwa kamati ya utendaji ya baraza la wafanya kazi, na kutatua changamoto mbalimbali kwa kufanya majadiliano yenye tija na kufanikisha ushirikishwaji katika vikao vya kupandisha watumishi madaraja kila mwaka.

Bw. Chizua ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi kwa kuwapatia eneo la kufanyia biashara ili waweze kukuza mfuko wa chama na kupunguza utegemezi, kuruhusu na kuwezesha viongozi wa tawi kuhudhuria semina mbalimbali zilizowawezesha viongozi kufahamu na kujifunza mambo mbali mbali ya utumishi wa umma na kuwezesha wanachama na wafanyakazi kuhudhuria sherehe za Mei Mosi na siku ya Wanawake Duniani.