TMDA yaridhia PPE za Muhimbili ambazo uzalishaji wake umeongezeka kwa asilimia 400

Mafundi wa Kitengo cha Ushonaji Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa katika maandalizi ya awali ya ushonaji wa vazi la kujingiza na maambukizi PPE

Mafundi wa Kitengo cha Ushonaji Hospitali ya Taifa Muhimbili wakishona vazi la PPE

Muonekano wa vazi la PPE linaloshonwa Hospitali ya Taifa Muhimbili

Vazi la PPE likiwa katika hatua ya utasishaji

Vazi la PPE likiwa tayari kupelekwa kwa wateja ambao ni Hospitali mbalimbali nchini.


Na Sophia Mtakasimba

Uzalishaji wa vazi kinga linalovaliwa na watoa huduma ili kuhudumia wagonjwa walioambukizwa Corona umeongezeka kutoka mavazi 120 hadi kufikia 600 kwa siku sawa na ongezeko la 400% katika kipindi cha mwezi mmoja tangu lilipozinduliwa na Muhimbili Aprili 17, 2020.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari

“Mpaka sasa Hospitali imezalisha PPE 10,553 kati ya hizo 5,000 zimesambazwa MSD na nyingine katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vituo vya Afya, taasisi zisizo za kiserikali, hospitali binafsi, makampuni, Halmashauri za Wilaya na Manispaa nchini. Tunaendelea kupokea mahitaji mbalimbali kwani sasa uwezo wa kuzalisha tunao. Bei elekezi ya PPE moja ni TZS. 50,000”amesema Aligaesha 

Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ilitambua vazi hili kupitia barua yenye Kumb. Na. BC.248/383/01/13 ya tarehe 23 Aprili, 2020 hivyo kuiruhusu Hospitali kuendelea kushona na kufanya usambazaji kote nchini.

“Tunapenda kukufahamisha kuwa Mamlaka imepitia na kuridhia ombi lako la utambuzi wa nguo za kujikinga na maambukizi (coverall, shoe cover na apron) zinazotengenezwa na Muhimbili Tailoring Unit kwa kutumia malighafi ya nylon” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Bw. Aligaesha alisema kuwa kwa ithibati hiyo  utengenezaji na usambazaji wa vifaa hivi unazingatia matumizi na uhifadhi unaofuata kanuni za udhibiti wa vifaa tiba nchini, The Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (Control of Medical Devices) Regulation, 2015 kama ambavyo hospitali iliekezwa na TMDA.