Teknolojia mpya kuwanufaisha wagonjwa wa afya ya akili Muhimbili

Mkurugenzi wa Shahada za Awali wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wa pili kutoka kushoto, Prof. Erasto Mbugi akikabidhi msaada wa Miundombiunu ya Mfumo wa Kieletroniki kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru (kulia). Wengine ni wataalamu wa magonjwa ya afya ya akili pamoja na wataalamu wa Tehama.

Prof. Mbugi akieleza umuhimu wa teknolojia hiyo kwamba itawezesha upatikanaji wa taarifa za magonjwa ya afya ya akili.

Pichani ni miundobinu ya mfumo wa kieletroniki.


Na John Stephen

Matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) yameongezeka, huku teknolojia hiyo ikiwawezesha wataalamu wa saikolojia kufanya tafiti na kutoa tiba ya magonjwa ya afya ya akili.

Tanzania, Chile na Kosovo ni moja ya nchi ambazo zimenufaika na teknolojia mpya ya miundombinu ya mfumo wa kieletroniki ambao umetolewa na Switzerland kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Mkurugenzi wa Shahada za Awali wa MUHAS, Prof. Erasto Mbugi amesema hayo wakati akitoa msaada wa Miundombinu ya Mfumo wa Kieletroniki kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma ya magonjwa ya afya ya akili kwa watoto na vijana pamoja na kuwezesha utafiti wa magonjwa hayo.

Prof. Mbugi amesema teknolojia hiyo itawezesha hospitali kupata taarifa sahihi za magonjwa ya afya ya akili, utoaji wa matibabu pamoja na kuwawezesha wataalamu kufanya tafiti mbalimbali.

“Miundombinu ya mfumo huu wa kieletroniki utawawezesha wataalamu kufanya uchunguzi wa magonjwa ya afya ya akili na kutunza taarifa kwa ajili ya tafiti. Lengo kubwa hapa ni kuboresha huduma za magonjwa ya afya ya akili kwa watoto na vijana,” amesema Prof. Mbugi.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amewashukuru wataalamu wa magonjwa ya saikolojia kwa juhudi za kupata msaada huo kwa kuwa utakuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wa afya ya akili.

“Tuna ushirikiano mzuri kati ya Muhimbili na MUHAS, hivyo tunakaribisha uwekezaji mwingine kama huu ili tuweze kukabiliana na upungufu wa vifaa tiba katika Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili,” amesema Prof. Museru.

Msimamizi wa Mifumo ya Tehama wa Muhimbili, Bw. Salum Juma amesema gharama ya msaada huo ni zaidi ya TZS 10 milioni.