Taasisi ya Benjamin Mkapa yaajiri watumishi 575 wa kada za afya, 80 wapangiwa Muhimbili

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akizungumza na baadhi wataalamu wa afya waliopata ajira ya muda kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt. Ellen Senkoro akizungumza na na baadhi wataalamu wa afya waliopata ajira ya muda kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akizungumza na na baadhi wataalamu wa afya waliopata ajira ya muda kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa

Baadhi wataalamu wa afya waliopata ajira ya muda kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa wakimsikiliza Katibu Mkuu

Baadhi wataalamu wa afya waliopata ajira ya muda kupitia taasisi ya Benjamin Mkapa wakiwa kwenye picha ya pamoja na katibu mkuu

Katibu Mkuu akiwa kwenye picha ya pamoja na menejiment ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Afya


Na Sophia Mtakasimba & Angela Mndolwa

Taasisi ya Benjamin Mkapa Kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau wa maendeleo, wakiwemo Shirika la Irish Aid, UKAID-DFID na UNFPA, imeajiri watumishi wa  kada mbalimbali za afya 575 kwa muda wa miezi sita kuanzia mwezi Julai 2020.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ajira hizo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa wote waliochaguliwa kuajiriwa wamepewa kipaumbele hicho kwa kuwa walikuwa wanajitolea katika maeneo waliyopangwa hivyo basi, Serikali ikaona ni vyema kuwatumia katika mfumo rasmi kwa kipindi cha miezi sita.

“Napenda kuwasihi kuwa ni vyema kuzingatia maadili ya utumishi na kujitahidi kuwa mfano katika maeneo yenu mtakayokuwa mkifanya kazi. Uadilifu wenu katika utoaji wa huduma ni wa muhimu kwani mtakuwa ni kioo cha namna sekta yetu ya Afya inavyofanya kazi.” Amesema Prof. Mchembe

Prof Mchembe aliongeza kuwa wataalamu hao 575 wamependekezwa kupangwa katika maeneo yaliyopewa kipaumbele na Serikali katika kuongeza nguvu ya kuimarisha huduma za afya za kupambana na magonjwa ya maambukizi na yasiyo ya maambukizi ikiwemo pia ya milipuko hapa nchini, mfano COVID19

Jumla ya Halmashauri 72 zilizopo katika mikoa 13 imepewa kipaumbele ikiwemo Dar Es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Mara, Pwani, Dodoma, Arusha, Mtwara, Kigoma, Mwanza, Simiyu, Mbeya na Songwe. Mbali na mikoa hiyo 13 ya Tanzania bara, pia mradi utawezesha upangaji wa watumishi 21 kwa upande wa Tanzania Visiwani ambapo huo mchakato wake unaendelea ili kuweza kuzingatia taratibu za ajira za Tanzania Visiwani.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt. Ellen Senkoro  amesema kuwa Tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Mkapa takriban miaka 14 iliyopita, taasisi imeendelea kushirikiana na serikali, katika jitihada zake za kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi ikiwemo pia kupatia ufumbuzi wa kupunguza upungufu wa wataalamu wa afya, ambao mpaka sasa umekadiriwa kuwa ni wa asilimia 52 ya watumishi wote wanaohitajika hapa nchini.

Pia ameshukuru Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI kwa ushirikiano wao madhubuti na mkubwa sana walioutoa katika kufanikisha ajira hizo. 

“Napenda kukiri kuwa, tumepata ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha taratibu zote za ajira zinafuatwa” amesema Dkt. Senkoro

Dkt. Senkoro amesema kuwa watumishi hao 575 wanatoka katika fani 13 ambazo ni Mteknolojia Maabara  Mteknolojia Maabara Msaidizi, Tabibu ,Tabibu Msaidizi, Daktari II, Afisa Muuguzi Msaidizi, Afisa Muuguzi  Afisa Ustawi wa Jamii , Afisa Ustawi wa Jamii Msaidizi , Mteknolojia Dawa , Mteknolojia Maabara Msaidizi , Afisa Afya Mazingira, na  Afisa Afya Mazingira Msaidizi.

Akimkaribisha Katibu Mkuu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru alisema kuwa Muhimbili inayo furaha kufanya kazi na Taasisi ya Benjamin Mkapa ambapo kati ya watumishi 575 watakaopata ajira watumishi 80 wamepangiwa kufanya kazi Hospitali ya Taifa Muhimbili.