Serikali yazitaka Muhimbili na Mnazi Mmoja kudumisha ushirikiano.

Naibu Waziri wa Afya Mh. Harusi Suleiman akizungumza na wanamichezo katika hafla ya ufungaji wa tamasha la pasaka liliofanyika Zanzibar.

Baadhi ya wanamichezo wakikiliza neno kutoka kwa Naibu waziri wa Afya .

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi Dkt. Praxeda Ogweyo, akitoa neno la shukrani wakati wa kufunga tamasha hilo.


Na Abubakary Mahamoud Omary

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Harusi Suleiman amezitaka Hospitali ya Taifa Muhimbili MNH  na Mnazi Mmoja kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo ili kuwaenzi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Naibu Waziri Suleiman ametoa kauli hiyo katika hafla ya kuhitimisha tamasha la Pasaka   2019 lililofanyika Visiwani Zanzibar na kuhusisha timu za michezo za Muhimbili pamoja na Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani humo.

Akizungumza katika hafla hiyo amesisitiza kwamba timu hizo zimekuwa zikikutana kila mwaka kwa lengo la kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya pande hizo mbili ambapo mwaka jana tamasha hilo lilifanyika Tanzania Bara.

“Ndugu zangu tumefarijika kuja kututembelea katika pasaka hii tunaomba ushirikiano huu uendelezwe kwa faida ya pande zote mbili, pia kikubwa nilichofurahishwa kutoka kwenu ni nidhamu pamoja na maadili kwani hata katika michezo tunasisitiza nidhamu na maadili hakika mnastahili pongezi”. Amesema Naibu Waziri wa Afya Zanzibar.

“Lakini pia yapaswa kuwashukuru viongozi wetu ambao walianzisha muungano wetu ambao umetuwezesha kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo michezo hivyo hatuna budi kuwaenzi kwa kuendeleza na kuiboresha zaidi michezo hii ambayo ilianzishwa mwaka 1972”. Amesisitiza Mh. Suleiman.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi kutoka Muhimbili Dkt. Praxeda Ogweyo, amewapongeza wanamichezo wote walioshiriki katika tamasha la Pasaka 2019 na kueleza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ipo mstari wa mbele katika kuhakikisha michezo inaendelezwa katika taasisi hiyo na kutoa fursa kwa watumishi wengi kushiriki.