Serikali yaridhishwa na uwekezaji Muhimbili

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango Bw. Doto James (Katikati)akiwasili Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuzungumza na Menejimenti na kujionea uwekezaji uliofanyika hospitalini hapo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru na Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Muhimbili Dkt. Sufian Baruan.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango Bw. Doto James akizungumza na Menejiment ya Hospitali ya Taifa Muhimbili

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akizungumza

Baadhi ya wajumbe wa menejiment ya Muhimbili wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango akimsikiliza mmoja wa wangonjwa wenye tatizo la figo wanaosafishwa damu (Renal dialysis).

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango akipata maelezo ya huduma zinazotolewa katika wodi ya watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalumu (NICU).

Mtaalamu wa Tiba Radiolojia akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango (hayumo pichani) kuhusu ufanisi wa mashine maalumu inayotumika katoa tiba hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango akijionea maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa binafsi unaoendelea hospitalini hapo.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango akipata maelezo kuhusu kitengo cha huduma za dharura kwa watoto (Pediatric emergency)


Na Sophia Mtakasimba

Serikali imeridhishwa na uwekezaji uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwa unaendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James alipotembelea Muhimbili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika hospitalini hapo lakini pia kukutana na menejiment ya hospitali hiyo.

“Nimekuja hapa na baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Wizara kuzungumza na menejiment ya Muhimbili ili kuzifahamu changamoto kwa kutembelea na kujionea wenyewe baadhi ya maeneo ya hospitali hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili katika wasilisho lake ametupitisha kwenye baadhi ya mafanikio ambayo hospitali imeyafikia ikiwemo uanzishwaji wa huduma za kibingwa nchini ambazo ni  upandikizaji figo, upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia, na tiba radiolojia ambazo kwa ujumla wake zimesaidia sana kuokoa fedha nyingi za serikali.” Amesema Bw. James

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2015 hadi sasa safari za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi zimepungua kutoka wagonjwa 683 hadi wagonjwa 64  na kitendo hiki cha wagonjwa kupungua kimeokoa Tzs 329 Bilioni ambazo serikali ilikuwa inatumia kila mwaka.

Bw. James ameeleza pia namna ambavyo ameridhishwa na Madaktari Bingwa wanaopatikana Muhimbili kwa kuwa ndio tegemeo hata katika hospitali kubwa za binafsi nchini.

“Hospitali hii ina rasilimali iliyojitosheleza kabisa kwa upande wa madaktari bingwa na wabobezi ambao wanaotegemewa  ndani na nje ya nchi, tatizo ni vitendea kazi tu ambavyo havijitoshelezi. Mara kadhaa nimejaribu kwenda kutibiwa kwenye hospitali nyingine binafsi nje  ya hapa lakini wataalamu ninaokutana nao huko ni wa kutoka hapa tangu nigundue hivyo nimekuwa karibu sana na Muhimbili.” Amesema Bw. James

Hivyo amemuomba Mkurugenzi Mtendaji na Menejiment ya Muhimbili kuandaa utaratibu wa kuwajengea uwezo madaktari  ili kufanya utolewaji wa huduma za kibingwa uwe endelevu.

Kuhusu changamoto zinazoikabili hospitali ikiwemo majengo chakavu Bw. James amesema kuwa serikali imeshafanya tathmini na imewasilisha benki ya dunia kuona namna ambavyo wanaweza kupata mkopo rahisi wa uboreshaji wa hospitali ,lakini wakati huo huo  tayari serikali imeshatoa fedha kwa ajili wa ujenzi wa jengo la wagonjwa binafsi litakalokuwa na uwezo wa vitanda 200 .

Awali akimkaribisha katibu Mkuu , Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru alisema kuwa hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma za kibingwa nchini na kupunguza rufaa za wagonjwa kutibiwa nje ya nchi , imeboresha miundombinu ya kutolea huduma pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wazalendo.

Pia Prof. Museru alielezea changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali ikiwemo  idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji msamaha, uchakavu wa baadhi ya miundombinu pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa hospitali.