Serikali kutatua changamoto za wauguzi nchini

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mh. Dorothy Gwajima akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa katika kilele cha siku ya wauguzi duniani kilichofanyika Mei 12 katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika (MUCO) Mkoani Kilimanjaro.

Baadhi ya wauguzi wakiwa katika maandamono ya kuelekea katika viwanja vya Chuo cha Ushirika Mkoani Kilimanjaro ambapo yamefanyika maadhimisho hayo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania Bw. Sebastian Luziga akielezea baadhi ya changamoto zinazowakabili watumishi wa kada ya uuguzi na ukunga.

Msajili wa Baraza la wauguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) Bi. Agness Mtawa akiongoza wauguzi wakati wa kula kila kiapo cha uadilifu katika taaluma ya uuguzi na ukunga.

Baadhi ya wauguzi waliohudhuria hafla hiyo wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu Mh. Dorothy Gwajima akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu .

Baadhi ya wauguzi wa hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) waliohudhira maazisho hayo wakiwa katika picha ya pamoja.


Na Dorcas David

Serikali inatambua na kuthamini umuhimu na mchango mkubwa wa wauguzi katika jamii na kwamba ndio kada ya afya ambayo watumishi wake wanatumia muda mrefu kuhudumia mgonjwa hivyo imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazoigusa kada hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mh. Dorothy Gwajima ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa katika kilele cha maadhimisho ya  Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika Mei 12 kwenye viwanja vya Chuo Cha Ushirika Mkoani Moshi (MUCO) mkoani Kilimanjaro.

“Nimesikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la kuchelewa kwa muundo wa utumishi wa maendeleo ya kada ya uuguzi na ukunga na kutotambuliwa wauguzi wenye stashahada ya juu na wenye shahada ya uzamili (Wauguzi Bingwa), kutozingatia kianzia cha mshahara kwa wauguzi wenye shahada ya kwanza ukilinganisha na muda wao wa masomo,  hivyo basi naagiza Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora pamoja na Waziri wa Afya kupata ufumbuzi wa jambo hili kwa haraka” amesema Dkt. Gwajima akisoma hotuba ya Waziri Mkuu

Kuhusu suala la muundo wa utawala katika sekta ya afya kuongozwa na kada moja ameagiza waziri mwenye dhamana ya afya kulitatua kwa kubadilisha miongozo ili kuwe na muundo shirikishi kama ilivyo kwa nchi zingine na ameomba kupata taarifa ya utekelezaji wake  kabla ya kuhitimishwa kwa Bunge la Bajeti kwani masuala hayo alishayatolea maelekezo mwaka 2017 akiwa Mkoani Lindi.

“Pia kuna suala la ubora wa vyuo vya ukunga na uuguzi kutiliwa shaka kuhusu ubora wa elimu inayotolewa, taaluma hii ni nyeti hivyo ninaagiza Waziri wa Afya akae na Waziri wa Elimu kwa kushirikiana na wana taaluma ili kuona namna ya kuimarisha usimamizi wa vyuo hivyo pia mabaraza ya kitaaluma yasimamie ubora wa vyuo, waalimu na wakufunzi” amesema Dkt Gwajima .

Katika hatua nyingine  ameitaka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kuzingatia uwiano wa ajira na kuwa na maafisa wauguzi wa kutosha ili kuweza kuinua ubora wa huduma ya afya. 

Awali akisoma Risala ya Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Katibu Mkuu wa chama hicho Bw. Sebastian Luziga alisema kuwa kada za uuguzi na ukunga zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo muundo wa utumishi kutotambua wauguzi bingwa, muundo wa utawala katika sekta ya afya kuongozwa na kada moja, pamoja na maslahi madogo kwa watumishi wa shahada wa kada hiyo licha ya kutumia miaka minne darasani na mmoja katika mafunzo.

Siku ya uuguzi duniani huadhimishwa kila tarehe 12 Mei ambapo mwaka huu imefanyika katika viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi (MUCO) na ilibeba kauli mbiu isemayo “wauguzi: sauti inayoongoza, wekeza kwenye uuguzi na heshimu haki kwa manufaa ya afya kwa wote”, na imehudhuriwa na wauguzi kutoka sehemu mbalimbali nchini ikiwemo wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila)