Prof. Museru awataka watumishi tarajali kukidhi matarajio ya wananchi

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati wa wakuhitimisha mafunzo elekezi kwa watumishi tarajali yaliyoendeshwa kwa muda wa siku mbili Hospitali ya Mloganzila kulia ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi.

Baadhi ya washiriki wakifatilia mafunzo kwa makini

Daktari Bingwa wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Garvin Kweka akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa mabadiliko ya tabia katika mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi.

Afisa Uchunguzi Mwandamizi Kanda Maalum Mkoa wa Dar es salaam Bi. Grace Matunda akielezea maadili ya utumishi wa umma wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.

Afisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) manispaa ya Ubungo Bi. Zenath Hamis akiwasisitiza watumishi kujiepusha na vitendo vya rusha ili kuboresha huduma za afya na kujenga imani kwa wananchi.

Baadhi ya viongozi wa Hospitali ya Mloganzila na watumishi tarajali wakifatilia mada zilizowasilishwa kwenye mafunzo hayo.


Na Dorcas David

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imehitimisha mafunzo elekezi ya siku mbili kwa watumishi tarajali wa kada mbalimbali za afya yaliyolenga kuwakumbusha kuzingatia maadili ya kazi ili kukidhi matarajio ya wananchi.

Akihitimisha mafunzo hayo, yaliyofanyika katika Hospitali ya Mloganzila, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amewasisitiza watumishia kuzingatia na kusimamia misingi ya maadili ya umma na kanuni za utendaji kazi za utumishi wa umma.

“Nijukumu la kila mtumishi wa umma kufuata miongozo yote iliyowekwa na Serikali ili kutoa huduma bora kwa kila mwananchi,” amesema Prof. Museru. 

Akizungumzia maadili ya utumishi wa umma, Afisa Uchunguzi Mwandamizi Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Grace Matunda amewataka watumishi hao kutoa huduma stahiki kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuivunjia heshima Serikali ikiwemo ulevi, kufanya vurugu mahala pa kazi na kuomba au kupokea rushwa.

“Timizeni wajibu wenu kwa kukufuata taratibu na kanuni za utumishi wa umma bila kufanya upendeleo wa kikabila, kijinsia, kiitikadi za kisiasa na kitamaduni,” amesema Bi. Matunda.

Naye Afisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Manispaa ya Ubungo, amewasisitiza watumishi wa afya kijiepusha na vitendo vya rushwa kwani taasisi haitaweza kumvumilia mtumishi yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Pia, ametaja madhara yanayoweza kutokea endapo mtumishi atajihusisha na vitendo vya rushwa kuwa ni pamoja na mgonjwa kupoteza maisha, kusababishia hasara Serikali, huduma kutolewa chini ya kiwango na jamii kupoteza imani ya huduma zinazotolewa.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo huduma bora kwa wateja, maadili ya utumishi wa umma, kuzuia na kupambana na rushwa, utekelezaji wa hati ya ahadi ya uadilifu, utunzaji wa vifaa, kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na namna bora ya kuwasiliana mahala pa kazi.