Prof. Museru awataka wadau kuwekeza katika tafiti kukabiliana na Covid-19 nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akiwasilisha mada kuhusu utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 nchini katika Kongamano la 12 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki katika Kongamano la 12 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere wakimsikiliza Prof. Museru wakati akiwasilisha mada kuhusu utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19.

Watoa mada wakisikiliza maswali ya washiriki katika Kongamano hilo.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bi. Debora Bugali akiuliza swali katika Kongamano hilo.

Washiriki katika Kongamano la 12 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere.


Na John Stephen

Wadau wa afya nchini wametakiwa kuwekeza katika tafiti za kisayansi ili kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 sambamba na kubadilisha mtazamo wa kupambana na ugonjwa huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila, Prof. Lawrence Museru amesema hayo leo wakati wa Kongamano la 12 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere wakati akiwasilisha mada kuhusu utoaji wa huduma za afya kupitia sekta ya umma tangu kuibuka kwa Covid-19 nchini, Machi mwaka jana.

Prof. Museru amesema wadau wa afya nchini wanapaswa kuwekeza katika utafiti kwa kuwa baada ya kutokea kwa janga hili, nchi za Afrika zilitegemea mbinu mbalimbali za nchi za Magharibi za kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema ugonjwa huo, ulitikisa mfumo wa utoaji wa huduma kutokana na kutokuwepo kwa mifumo imara ya utafiti, upungufu wa wataalamu wa afya pamoja na kutokuwepo kwa vifaa tiba vya kutosha katika vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.

Mkurugenzi huyo amesema kuwepo kwa ugonjwa huo hapa nchini kulisababisha gharama za utoaji huduma kuwa juu kwani gharama za barakoa zilipanda kipindi hicho, kulikuwa na upungufu wa dawa kutokana na nchi nyingi kuzuia dawa kutoka nchini kwao wakati huohuo sekta ya usafirishaji nayo ilipata changamoto baada ya nchi nyingi kufunga mipaka.

 Prof. Museru anabainisha kwamba mbali ya Covidi-19 kusababisha gharama za utoaji huduma kuwa juu wakati huo, pia ugonjwa huo ulisababisha hofu kwa jamii, unyanyapaa, wagonjwa wengine walijitenga majumbani na kupoteza maisha. 

“Watoa huduma nao waliathirika kisaikolojia kwani walipata hofu ya kuambukizwa Covidi-19 pamoja na familia zao,” amesema Prof. Museru.

Prof. Museru ameiomba Serikali kudhibiti  gharama za uzalishaji wa vifaa tiba na  bidhaa nyingine za afya ili kupunguza gharama za utoaji wa huduma za tiba nchini.