‘Nilikuwa siwezi kuzungumza wala kufanya chochote, nawashuru wataalamu Muhimbili’

Bw. Chile Thomas Kutibila akikata keki ambayo ni zawadi aliyopatiwa na wataalamu wa wodi sita, Jengo la Mwaisela.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Dkt. Mohamed Mnacho akizungumza wakati wa kumuaga Bw. Kutibila.

Baadhi ya wataalamu wakiwa katika hafla ya kumuuaga mgonjwa huyo.

Kiongozi wa wodi namba sita katika Jengo la Mwaisela, Bw. Odillo Byabato akizungumza kabla ya kumruhusu Bw. Kutibila kurejea nyumbani.

Wataalamu wakiwa katika picha ya pamoja na Bw. Kutibila.


Na John Stephen

 

Mgonjwa Chile Thomas Kutibila ambaye alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa miezi minane, huku akiwa amepoteza fahamu kwa miezi minne, sasa ameruhusiwa kurejea nyumbani mkoani Kigoma baada ya afya yake kuimarika.

Bw. Kutibila alikuwa akisumbuliwa na maradhi sugu ya mishipa ya fahamu na kusababisha kushindwa kuzungumza na pia alikuwa hawezi kushika chochote, huku akishindwa kutembea.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Dkt. Mohamed Mnacho amesema baada ya Bw. Kutibila kupatiwa matibabu kwa muda wa miezi minne alipata fahamu na mikono ilianza kufanya kazi, huku miguu yake ikiendelea kuimarika pole pole.

“Kutibila alifanyiwa uchunguzi kwa kutumia vipimo mbalimbali na ilibainika kwamba alikuwa na maradhi sugu ya mishipa ya fahamu na kuanzishiwa matibabu haraka,” amesema Dkt. Mnacho.

Naye, Kiongozi wodi namba sita katika Jengo la Mwaisela, Bw. Odillo Byabato amesema baada ya mgonjwa huyo kupata nafuu alisema yeye ni mkazi wa Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Tarafa ya Nyakitonto, Kijiji cha Mgombe, huku akibainisha kuwa hana baba wala mama na kwamba ana ndugu wawili ambao ni kaka na dada yake.

“Hospitali ya Muhimbili iliwasiliana na Mtendaji wa Kijiji cha Mgombe ambaye alisaidia kumpata kaka yake, Bw. Banyanga Thomas ambaye aliomba hospitali iwasaidie kumrejesha nyumbani kwao Mgombe,” amesema Bw. Byabato.

Bw. Byabato amesema ombi la ndugu wa mgonjwa limefanyiwa kazi na atapelekwa hadi nyumbani kwao katika Kijiji cha Mgombe, huku akisindikizwa na muuguzi.

Akizungumza baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani, Bw. Kutibila aliishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili na Serikali kwa msaada wa matibabu aliopata katika kipindi cha miezi minane aliyokuwa amelazwa.  

“Nashukuru madaktari na wauguzi kwa matibabu mazuri, nilivyoletwa hapa nilikuwa siwezi kuzungumza wala kutembea, mikono na miguu ilikuwa haiwezi kufanya kazi, lakini sasa naweza kuzungumza na kula chakula,” amesema Bw. Kutibila.

Mkuu wa Idara ya Uuguzi, Bw. Yassin Munguatosha alimtakia safari njema ya kurejea nyumbani kuungana na ndungu zake.