Muhimbili yazindua utafiti kubaini saratani kwa kutumia teknolojia ya kisasa

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Hedwiga Swai akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa utafiti unaolenga kuboresha utambuzi na matibabu ya saratani za damu kwa watoto.

Baadhi ya wataalamu wa afya kutoka taasisi mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa kuzindua mradi huu ambao umefanyika MNH.

Profesa wa Hematolojia kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Prof. Anna Schuh akizungumza kwenye uzinduzi wa kutafiti jinsi kutibu saratani za damu kwa watoto kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Baadhi ya wataalamu wa afya kutoka taasisi mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi huo.

Mtaalamu wa patholojia kutoka Hospitali ya KCMC, Dkt. Alex Mremi akitoa mada kwenye mkutano wa uzinduzi wa utafiti huu.

Wataalamu wakiwa kwenye uzinduzi wa utafiti huu leo.

Baadhi ya wataalamu wakiwa katika picha ya pamoja baada uzinduzi wa utafiti jinsi kutibu saratani za damu kwa watoto kwa kutumia teknolojia ya kisasa.


Na Sophia Mtakasimba

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imezindua mradi wa utafiti unalenga kuboresha utambuzi na matibabu ya saratani za damu kwa watoto  ambao utashirikisha Chuo kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS), Hospitali ya KCMC, Hospitali ya St. Mary’s ya Uganda pamoja na Shirika la Tumaini la Maisha.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Hedwiga Swai amesema kuwa utafiti huo unakusudia kutafuta njia rahisi ya kugundua saratani ya damu aina ya  Epstein-Barr Virus-lymphomas inayosababishwa na virusi vinavyopatikana zaidi maeneo ya kusini mwa Jangwa la Sahara.


“Kwa sasa ili kugundua saratani hii inabidi mgonjwa apitie mchakato wa zaidi ya wiki mbili unaohusisha kuchukuliwa  sampuli ya kinyama ambacho  kinapelekwa maabara na baada ya majibu kutoka wataalamu wa patholojia wanayatafsiri, hivyo mradi huu ni wa manufaa sana kwa sababu unatafuta namna rahisi ya uchukuaji wa sampuli ya damu na upimaji wa vinasaba,” amesema Dkt. Swai.


Dkt. Clara Chamba, Mchunguzi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba Muhumbili, amesema wanatafuta namna ya kuchunguza na kutibu kansa hiyo kwa haraka ili mtoto aweze kupata tiba ambayo ni kutoa damu na kwenda kupima vinasaba ili kubaini uwepo wa virusi vinavyosababisha saratani.


Dkt. Clara amesema kuwa hiyo itapunguza muda wa mgonjwa kusubiria majibu kutoka wiki mbili hadi siku moja, lakini pia itasaidia uchukuzi kufanyika hata hospitali za kawaida tofauti na sasa ambapo uchunguzi unafanyika kwenye hospitali za taifa.


Profesa wa Hematolojia kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Prof. Anna Schuh anayeongoza utafiti huo amesema kuwa anaamini teknolojia Ya upimaji wa vinasaba kwenye damu kwa kutumia patholojia ya kidijitali utarahisisha uchunguzi na matibabu ya saratani ya damu kwa watoto  na kama mradi huu ukifanikiwa vipimo hivyo vinaweza kusaidia kupima aina nyingine za saratani.


Mradi huu ni wa miaka minne una thamani ya shilingi bilioni 13.5 na unafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Taasisi ya Utafiti wa Afya(National Institute for Health Research-UK) na kampuni mbalimbali za nchini Uingereza ambayo yatasaidia kupatikana kwa vifaa vya utambuzi wa saratani hiyo.