Muhimbili yazindua ICU mbili za watoto wachanga, zapunguza vifo

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof Charles Majinge akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa ICU mbili za watoto wanaohitaji uangalizi maalumu PICU na NICU. Kulia ni Mwakilishi wa Malkia wa Sharja, Dkt. Sawsan Abdul Salam Al Madhi akishiriki katika uzinduzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Tumaini la Maisha (TLM), Bw. Gerald Mongella akishuhudia tukio hilo. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Dkt. Ellen Senkoro naye akishudia tukio hilo leo. Mke wa Mfalme wa UAE, Shaikha Jawaher Bint Mohammed AlQasim amefadhili ujenzi wa wodi mbili za watoto chini ya siku 28 na kuanzia umri wa mwaka mmoja kuendelea kwa thamani ya shilingi bilioni 4.9.

Mojawapo ya ICU ya watoto wenye umri wa siku 29 hadi miaka 14 iliyozinduliwa leo.

Mwakilishi wa Malkia wa Sharja, Dkt. Sawsan Abdul Salam Al Madhi akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kabla ya kuzinduliwa kwa ICU mbili za watoto wanaohitaji uangalizi maalumu ya PICU na NICU. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Dkt. Ellen Senkoro.

Baadhi ya wataalamu wa afya wa MNH wakishiriki katika uzinduzi wa ICU mbili za watoto wanaohitaji uangalizi maalumu ya PICU na NICU.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Prof. Charles Majinge akizungumza na wataalamu wa afya kabla ya uzinduzi wa wodi hizo. Kulia ni Mwakilishi wa Malkia wa Sharja, Dkt. Sawsan Abdul Salam Al Madhi na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai wakimsikiliza Prof. Majinge.

Wataalamu na wajumbe wa Tumaini La Maisha (TLM) wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa ICU za watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai akizungumza katika shughuli hiyo ya uzinduzi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi wa TLM, Bw. Gerald Mongella, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Dkt. Ellen Senkoro na wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Prof. Majinge na Mwakilishi wa Malkia wa Sharja.

Mwenyekiti wa Bodi wa TLM, Bw. Gerald Mongella akifafanua jambo kwenye mkutano wa uzunduzi wa ICU mbili za watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.

Baadhi ya wataalamu wa MNH na wajumbe wa TLM wakiwa kwenye mkutano leo.

Daktari Bingwa wa Watoto na Mkuu wa Kitengo cha Watoto Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (PICU), Dkt. Yasser Habresh Said akimweleza Mwakilishi wa Malkia wa Sharja, Dkt. Sawsan Abdul Salam Al Madhi, huduma zinazotolewa katika ICU hiyo. Katikati Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Prof. Majinge.


Na John Stephen


Tanzania ni nchi mojawapo duniani iliyofanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili na imesababisha kufikia mpango namba nne wa malengo ya millennia.

Mafanikio haya yamekuja baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Tumaini la Maisha (TLM) kujenga ICU mbili za watoto wanaohitaji huduma za uangalizi maalumu. Kutokana na juhudi hizo, Muhimbili imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto waliokuwa wanahitaji uangalizi maalumu kutoka asilimia 70 ya vifo vilivyokuwa vikitokea ndani ya saa 24 na kufikia asilimia 30.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru wakati wa uzinduzi wa ICU  zinazowahudumia watoto wanaohitaji uangalizi maalumu chini ya umri wa siku 28 (Neonatal Intensive Care Unit) na watoto wenye umri wa kati ya mwezi mmoja hadi miaka 9 (Pediatric Intensive Care Unit) zenye dhamani ya shilingi bilioni 4.9 zilizojengwa kwa ufadhili wa Mke wa Mfalme wa UAE, Shaikha Jawaher Bint Mohammed AlQasim kupitia Shirika la Tumaini la Maisha (TLM).

“Hospitali ya Taifa Muhimbili ndiyo Hospitali kubwa kuliko hospitali zote nchini, idara ya watoto wenye umri siku 0 mpaka 28 kina vitanda (baby cots) 134 na umri wa siku 29 mpaka miaka 14 kina vitanda 294 na ndicho kitengo chenye vitanda vingi nchini. Kitengo hiki kinahudumia watoto wote wanaozaliwa Muhimbili na wanaoletwa kwa njia ya rufaa kutoka takribani hospitali zote za mikoa nchini,” amesema Dkt. Swai 

Dkt. Swai amesema kwa kipindi kirefu watoto walikua hawana ICU maalumu kwa ajili yao hivyo kulazwa  ICU ya kawaida ya watu wazima hali iliyosababisha watoto hao kukosa huduma muhimu.
 
“Uwepo wa ICU hizi maalumu kwa watoto utafanya watoto waweze kuonwa kwa ukaribu na madaktari na wauguzi waliobobea katika kutoa huduma stahiki kwa watoto tofauti na awali ambapo watoto walichanganywa kwenye ICU za watu wazima,” amesema Dkt. Swai.

Pia, amesema katika kuendelea kutekeleza maazimio ya mpango namba nne wa milenia wa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, Muhimbili imefanikiwa kuwa na muongozo wake wa kutoa huduma kwa watoto wachanga na watoto chini ya miaka 14 (PICU Guidelines).

“Haya ni mafanikio makubwa sana kwani tumefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka asilimia 19.2 mwaka 2017/2018 mpaka asilimia 16.2 mwaka 2018/2019. Haya ni mafanikio makubwa kwetu katika kipindi cha mwaka mmoja,” amesema Dkt. Swai.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Charles Majinge ameshukuru Shirika la Tumaini la Maisha (TLM) na malkia wa Sharja kwa msaada huo, pia ameutaka uongozi wa Muhimbili kuhakikisha hizi ICU zinatunzwa ili watoto wote watakaopitia hapo waweze kunufaika na huduma za uangalizi maalumu.