Muhimbili yapokea Msaada wa Vifaa vya Fiziotherapia

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati akipokea msaada wa vifaa tiba kwa wagonjwa wa himofilia na selimundu. Msaada huo unalenga kuboresha tiba ya fiziotherapia na utengamao.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.

Prof. Museru akikata utepe ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa huduma za fiziotherapia na utengamano kwa wagonjwa wa himofilia na selimundu. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Utengamao wa MNH, Bw. Abdalla Makala na kushoto ni Daktari Bigwa wa Magonjwa ya Damu, Bi. Stellah Rwezaula.

Mkuu wa Idara ya Utengamao MNH, Bw. Makala akipokea cheti kutoka kwa Prof. Lawrence Museru.


Na Angel Mndolwa

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vifaa tiba vya fiziotherapia vyenye thamani ya shillingi TZS 84 Mil. kutoka katika mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji huduma kwa magonjwa ya damu unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania na Kenya kwa  ufadhili wa Novo Nordisk Haemophilia Foundation (NNHF)  na Novo Nordisk Foundation (NNF).

Msaada huo ambao unalenga kuboresha tiba ya fiziotherapia na utengamao (Physiotherapy and Physical Rehabilitation) kwa wagonjwa wa himofilia na selimundu nchini umeambatana na mafunzo kwa wataalamu 34 wa fiziotherapia na utengamao kutoka hospitali 26 nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amewashukuru wafadhili wa mradi huo na kuwataka wataalamu wa Fiziotherapia kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kuleta tija katika matibabu ya wagonjwa wa Himofilia na Selimundu.

“Ninafahamu kuwa mradi huu, utaendelea kuboresha huduma za Fiziotherapia katika hospitali za Kanda na mikoa nchini, hivyo ni matumaini yangu kuwa sisi tuliohudhuria mafunzo haya tutapeleka elimu kwa wengine katika maeneo yenu ya kazi,” amesema Prof. Museru.

Mkuu wa Idara ya Utengamao MNH, Bw. Abdalla Makala amesema kuwa Tiba ya fiziotherapia na utengamao huwasaidia wagonjwa wa himofilia kupunguza maumivu ya misuli na viungo na pia kupunguza uwezekano wa kupata ulemavu kutokana na changamoto ya kuvilia kwa damu kwenye viungo au misuli kwa kuwa Mfiziotherapia hutumia namna mbalimbali katika kutoa matibabu ikiwemo vifaa vya umeme (electrotherapy), barafu, mazoezi tiba, ushauri na utoaji elimu kuhusu namna bora ya kuepusha matatizo tajwa.