Muhimbili Yapokea Msaada wa Vifaa Tiba


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wenye thamani ya shilingi milioni kumi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bi. Nuru Mhando amesema mamlaka hiyo inatambua na kuthamini dhamira na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufikisha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wote hivyo imeamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa msaada wa viti vya kubebea wagonjwa na vipima joto vya kisasa .

‘’Kwa kutambua hilo mamlaka imeona ni vyema iunge mkono juhudi hizi katika wiki hii ambayo tupo kwenye shamrashamra za kuadhimisha miaka kumi na tatu tangu TPA ianzishwe, Aprili 15 ,2005, Mamlaka imeona ni vyema kusheherekea kumbukumbu hizi kwa kutoa mchango huu ili kusaidia wagonjwa katika jengo la watoto.

‘’Tunaamini msaada huu utasaidia kuhudumia watoto wengi kwa wakati mmoja na hivyo kutatua changamoto ya ukosefu wa vifaa hivi ambavyo mnakabiliana navyo,’’amesema Kaimu Mkurugezi huyo wa TPA.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za uuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Agness Mtawa ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, amesema msaada huo utaongeza kasi ya utoaji huduma kwa watoto.

Amefafanua kwamba jengo la watoto lina vitanda takribani 300 hivyo mahitaji ya viti vya kubebea wagonjwa pamoja na mahitaji mengine ni makubwa.

“Tunawashukuru TPA kwa msaada huu mliotupatia , mmeongeza kasi ya utoaji huduma niwahakikishie kwamba msaada huu utatumika kama ambavyo imekusudiwa,’’amesema Mkurugenzi Mtawa.

Ametoa rai kwa wadau wengine kujitokeza kuchangia huduma za afya na kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma hizo

Muhimbili yapokea msaada wa vifaa tiba

Mratibu wa Mafunzo ya Kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto wa Global Health Alliance Western Australia (GHAWA), Bi. Salem Tesgalul akikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Mkuu wa Idara ya Uuguzi na Ukunga wa Muhimbili, Bi. Mugara.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya TZS 3 milioni kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya katika hospitali hiyo. Msaada huo umetolewa na Global Health Alliance Western Australia (GHAWA) baada ya kutoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga 390 wa MNH kunzia mwaka 2011 hadi 2020.

Mratibu wa Mafunzo ya Kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto, Bi. Salem Tesgalul amesema vifaa tiba hivyo vitatumika kuwafundisha wauguzi wengine ambao hawakupata nafasi ya kupatiwa mafunzo hayo. Amesema baadhi ya msaada wa vifaa tiba ni aprone, sphygmomanometer na splash shield.