Muhimbili yapokea msaada wa mashine ya Patholojia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya (katikati) akizindua mashine ya kusaidia kusoma vipimo vya histopatholojia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo imetolewa msaada na wataalamu wa Patholojia kutoka nchini Marekani, Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru akishuhudia uzinduzi huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kupokea msaada wa mashine ya kisasa kwa ajili ya kusoma vipimo vya histopatholojia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru na Mkurugenzi wa Kituo cha Afya kutoka Taasisi ya wataalumu wa Patholojia nchini Marekani, Dkt. Danny Milner.

Baadhi ya wataalamu wa patholojia na waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Ulisubisya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mashine hiyo.

Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Leah Mnango akieleza jinsi mashine hiyo inavyofanya kazi. Kutoka kushoto ni Prof. Museru, Katibu Mkuu wizara ya Afya, Dkt. Ulisubisya na wataalamu kutoka Taasisi ya wataalumu wa Patholojia nchini Marekani.

Mkurugenzi wa Kituo cha Afya kutoka Taasisi ya wataalumu wa Patholojia nchini Marekani, Dkt. Danny Milner akieleza uwezo na jinsi inavyorahisisha kusoma vipimo vya histopatholojia.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa mashine ya Patholojia kutoka kwa wataalam nchini Marekani ambayo itasaidia kurahisisha utoaji wa majibu ya wagonjwa wa saratani kutoka siku 14 hadi siku 3.

Mashine hiyo ambayo imegharimu Tshs. 308,340,000 milioni, itasaidia kutunza majibu ya vipimo katika mfumo wa kisasa na kwa ubora zaidi na kumsaidia mtaalam wa Patholojia kuwa na uwezo wa kusoma majibu hayo kupitia kompyuta yake mahali popote.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo leo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto,  Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema mashine hiyo itarahisisha wataalam 18 wa Patholojia nchini kujua njia sahihi ya kutibu saratani huku wakishirikiana na wataalam kutoka nje ya nchi.

 “Kutakuwa na faida ya uhifadhi wa vipimo kwa kipindi kirefu ili kuondoa upotevu wa vipimo, hivyo majibu ya vipimo yatakuwa yatahifadhiwa kisasa na pia itaongeza ufanisi wa ugunduzi wa magonjwa ya saratani,” amesema Dkt. Ulisubisya. 

Mkurugenzi Mtendaji wa (MNH) Prof. Lawrence Museru amewashukuru wataalamu hao kwa kutoa msaada huo kwani utasaidia kutatua changamoto ya kupunguza msongamano wa wagonjwa wakati wa kusubiri majibu ya vipimo na hivyo kuwezesha matibabu kuanza kwa wakati.

Prof. Museru amesema mashine hiyo itasaidia kuboresha huduma za vipimo vya saratani na hivyo wagonjwa kunufaika huduma zinazotolewa Muhimbili.