Muhimbili yaongoza matibabu ya watoto njiti nchini, yakabidhiwa hundi ya Tzs 100 milioni

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi akizungumza katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mbio za kilometa 21, 10 na kilometa 5. Mbio za kilometa 5 zilianzia Mlimani City na kumalizikia Geti la Maji, kilometa 10 zilianza Mlimani City na kumalizika Mwenge na kilometa 21 Kawe.

Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila wakikimbia mbio za kilometa tano.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Upanga, Prof. Museru akizungumza katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam.

Washiriki wakikimbia mbio za kilometa 10.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru akipokea hundi ya Tzs. 100 mil kwa ajili ya kununua vifaa vya watoto njiti.

Prof. Museru akipokea medali baada ya kumaliza mbio za kilometa tano

Picha ya pamoja ya watumishi wa Muhimbili Upanga na Mloganzila.

Watumishi wa Muhimbili-Mloganzila wakiwa pamoja baada ya kumaliza mbio za kilometa tano na kilometa 10.

Watumishi wa Muhimbili Upanga na Mloganzila.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Makubi akiwa na baadhi ya washindi wa Bima Marathoni.


Na Priscus Silayo

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kuongoza katika matibabu ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti) hapa nchini.

Prof. Makubi amesema hayo leo alipokua akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mh. Kassim Majaliwa katika mbio maalumu za Bima Marathoni za kuwezesha upatikanaji wa Tzs. 100 mil. ambazo zitatumika kununua vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia watoto njiti. Mbio hizo  zilianzia katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam na zilikuwa za kilometa tano, kumi na 21.

Amebainisha kwamba asilimia 13 hadi 17 ya watoto wanaozaliwa hapa nchini ni njiti hivyo wanahitaji uangalizi maalumu ili waweze kukua vizuri.

"Watoto hawa huathiriwa pia na magonjwa ya maambukizi ya bakteria au kushindwa kupumua baada ya kuzaliwa na kuchangia asilimia 80 ya vifo vyote vya watoto wachanga na kuongeza kuwa dozi moja ni Tzs. 600,000" amesema Prof. Makubi.

Pia, Prof.  Makubi ametumia fursa hiyo kuwashauri Watanzania kukata bima na kujenga mazoea ya kufanya mazoezi ili kuwa na afya bora.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amekabidhi mfano wa hundi ya Tzs. 100 mil. kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kununua vifaa vya matibabu ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti).

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga & Mloganzila, Prof. Lawrence Museru amesema Muhimbili inapokea watoto njiti 20 kila siku idadi ambayo inajumuisha wanaozaliwa Hospitali ya Muhimbili na wanaozaliwa  katika Mkoa wa Dar es Salaam na Hospitali za rufaa nchini.

Amesema kutokana na hali hiyo  imeilazimu hospitali kuongeza wodi za watoto wachanga, kuboresha huduma za watoto wachanga mahututi kwa kuanzisha ICU ya watoto wachanga ( Neonatal ICU) yenye vitanda saba na vitanda 13 vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu sanjari na kuwapatia mafunzo wahudumu wa afya ili waweze kukidhi mahitaji ya wodi hiyo.

Kwa upande wake mama aliyejifungua watoto wanne kabla ya muda amewashauri wadau mbalimbali kuendelea kuchangia vifaa kwani matibabu ya watoto njiti ni  ghali na  wanahitaji uangalizi wa karibu.

Mbio za Bima Marathoni zinafanyika kwa mara ya pili ambapo mwaka jana Tzs. 100 mil. zilikusanywa kwa ajili ya kugharamia matibabu ya Saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.