MUHIMBILI YAHUDUMIA WANANCHI 385 SABASABA, 30 WAPEWA RUFAA

Daktari wa Magonjwa ya dharura Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Lawanna Msilawova akitoa huduma ya matibabu kwa mmoja wa washiriki wa sabasaba aliyetembelea banda la Muhimbili kupata huduma.

Mtaalamu wa Optometria Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bi. Paulina Mvella akitoa huduma ya Macho kwa mmoja wa washiriki aliyetembelea banda la Muhimbili kupata huduma.

Baadhi wa washiriki waliotembelea Banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga & Mloganzila wakisubiri huduma.


Na Sophia Mtakasimba

 

Jumla ya wananchi 385 wamepata huduma za uchunguzi wa macho, saratani ya matiti na huduma za dharura katika banda la Muhimbili  kwenye maonyesho ya 44 ya Sabasaba tangu yalipoanza Julai Mosi mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha wakati akielezea muitikio wa wananchi wanaotembelea banda la Muhimbili.

Amesema kuwa kati ya wananchi hao, 214 wameonwa kwenye kliniki ya macho, 56 kliniki ya saratani ya matiti na 115 kupitia idara ya magonjwa ya dharura.

Wananchi 30 wamepewa rufaa  ya matibabu zaidi katika Hospitali za Muhimbili zilizopo Upanga na Mloganzila.

"Wananchi 51 wamepata miwani ya kusomea ambayo inapatikana hapahapa katika banda letu la sabasaba kuchangia gharama kidogo ya TZS. 10,000, amesema" Bw. Aligaesha.

Bw. Aligaesha ametoa wito kwa wananchi wanaotembelea maonyesho hayo waendelee kufika kwenye banda la Muhimbili kupimwa afya zao bila malipo kwani lengo la Hospitali ya Taifa Muhimbilini kuhakikisha inawafikia wananchi.