Muhimbili kujenga kituo maalum cha kupandikiza viungo

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu MNH kutimiza miaka miwili tangu ianze kupandikiza figo mwaka 2017 kwa wagonjwa mbalimbali waliokuwa wakihitaji huduma hii. Wengine ni wataalam wa MNH wakiwamo wagonjwa waliopandikiwa figo pamoja na ndugu waliowachangia figo wagonjwa.

Mkazi wa Morogoro, Bi. Prisca Mwingira ambaye alikuwa mgonjwa wa kwanza kupandikizwa figo mwaka 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu maendeleo ya afya yake baada ya kupatiwa huduma hii.

Bw. Juma Kanzaga (70), mkazi wa mkoani Mara akieleza jinsi alivyomchangia figo mtoto wake Bw. Omary Juma (47).

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Museru akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa MNH wakiwamo wagonjwa waliopandikizwa na waliochangia figo.


Na Sophia Mtakasimba

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina mpango wa kujenga kituo maalum cha kupandikiza viungo (Transplant centre) katika Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru amesema kuwa lengo la kujengwa kwa jengo hili ni kuboresha huduma za kupandikiza viungo ikiwemo upandikizaji figo, upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia, huduma ya upandikizaji uloto na upandikizaji mimba kwa watu waliokosa watoto inayotarajia kuanza hivi karibuni.
Prof. Museru amesema kutokana na juhudi za wataalam wa MNH, mpaka sasa wagonjwa 51 tayari wamepandikizwa figo na kwamba upasuaji ulifanyika kwa gharama nafuu na kuwanufaisha wananchi.
“Hapa nchini huduma hii kwa mtu mmoja inafanyika kwa Shilingi milioni 30 wakati nje ya nchi ni shilingi milioni 100 hadi 120. Tumetumia shilingi bilioni 1.53 hadi sasa kwa wagonjwa 51 waliofanyiwa upasuaji. Kama wangelifanyiwa nje ya nchi zingetumika shilingi bilioni 6.120.Hivyo tumeokoa shilingi 4.590 bilioni,” amesema Prof. Museru.
Akizungumzia mipango ya baadaye, Prof. Museru amesema kwamba MNH baada ya huduma ya upandikizaji Figo kuhimarika sasa Hospitali itaanza upandikizaji Figo kwa kundi la watu wenye vihatarishi vya juu (high risk) ikiwemo kundi la watu ambao siyo ndugu kama Mume na Mke na watu wenye maambukizi kama HIV na Hepatitis B
Pia, Prof. Museru amewapongeza wataalam wabobezi wa figo, upasuaji, ICU, radiolojia, maabara na wataalam wa lishe.